1 Sam. 22:10-23 Swahili Union Version (SUV)

10. Naye akamwuliza BWANA kwa ajili yake, akampa vyakula, akampa na ule upanga wa Goliathi, Mfilisti.

11. Ndipo mfalme akatuma watu waende kumwita Ahimeleki, kuhani, mwana wa Ahitubu, na jamaa yote ya baba yake, hao makuhani, waliokuwako huko Nobu; nao wakaenda kwa mfalme wote pia.

12. Sauli akasema, Sikia sasa, Ewe mwana wa Ahitubu. Naye akaitika, Mimi hapa, bwana wangu.

13. Sauli akamwuliza, Mbona mmefanya fitina juu yangu, wewe na mwana wa Yese? Kwa maana umempa mikate, na upanga, nawe umemwuliza Mungu kwa ajili yake, ili aniondokee na kunivizia kama hivi leo?

14. Basi Ahimeleki akamjibu mfalme, akasema, Katika watumishi wako wote ni nani aliye mwaminifu kama Daudi, aliye mkwewe mfalme, tena msiri wako, mwenye heshima nyumbani mwako?

15. Je! Mimi nimeanza leo tu kumwuliza Mungu kwa ajili yake? Hasha! Mfalme asinidhanie mimi, mtumishi wake neno hili, Wala jamaa yote ya baba yangu, kwa maana mimi, mtumishi wako siyajui hayo yote, yaliyopungua au yaliyozidi.

16. Naye mfalme akasema, Kufa utakufa, Ahimeleki, wewe na jamaa yote ya baba yako.

17. Kisha mfalme akawaambia askari walinzi waliosimama karibu naye Geukeni, mkawaue hao makuhani wa BWANA, kwa sababu mkono wao u pamoja na Daudi, na kwa sababu walijua ya kuwa amekimbia, wasiniarifu. Lakini watumishi wa mfalme walikataa kunyosha mkono na kuwaangukia makuhani wa BWANA.

18. Basi mfalme akamwambia Doegi, Geuka wewe, ukawaangukia hao makuhani. Basi Doegi, Mwedomi, akageuka, akawaangukia makuhani, akaua siku ile watu themanini na watano wenye kuvaa naivera ya kitani.

19. Kisha akaupiga Nobu, mji wa makuhani, kwa makali ya upanga, wanaume na wanawake, watoto na wanyonyao, na ng’ombe, na punda, na kondoo.

20. Na katika wana wa Ahimeleki, mwana wa Ahitubu, akaokoka mtu mmoja tu, aliyeitwa jina lake Abiathari, akamkimbilia Daudi.

21. Naye Abiathari akamweleza Daudi ya kwamba Sauli amewaua makuhani wa BWANA.

22. Daudi akamwambia Abiathari, Siku ile alipokuwako Doegi, Mwedomi, nalijua yakini ya kuwa atamwambia Sauli; mimi nimewapatia watu wote wa jamaa ya baba yako kifo.

23. Kaa wewe pamoja nami, usiogope; kwa maana yeye atafutaye roho yangu, ndiye atafutaye na roho yako; nawe utakaa kwangu salama.

1 Sam. 22