5. Naye Daudi akamwambia Yonathani, Tazama, kesho ni mwandamo wa mwezi, nami hainipasi kukosa kuketi chakulani pamoja na mfalme; lakini niache nijifiche bondeni hata siku ya tatu jioni.
6. Baba yako akiona ya kuwa sipo basi sema, Daudi alitaka sana nimpe ruhusa, aende upesi Bethlehemu, mji wake, kwa maana iko huko dhabihu ya mwaka kwa ajili ya jamaa yake yote.
7. Basi, akisema, Ni vema, mimi mtumishi wako nitakuwa na amani; bali akikasirika, ujue ya kuwa amekusudia kutenda jambo baya.
8. Basi, unitendee mema mimi mtumishi wako; kwa sababu umenitia mimi mtumishi wako katika agano la BWANA pamoja nawe, lakini ikiwa mna uovu moyoni mwangu, uniue wewe mwenyewe; kwa nini kunileta kwa baba yako?
9. Naye Yonathani akasema, Haya na yawe mbali nawe, kwa maana kama ningejua ya kuwa baba yangu amekusudia kukutenda neno baya, je! Singekuambia?
10. Basi Daudi akamwambia Yonathani, Ni nani atakayeniambia, ikiwa baba yako amekujibu maneno makali?
11. Yonathani akamwambia Daudi, Twende zetu nje mashambani. Wakatoka wote wawili, wakaenda mashambani.
12. Naye Yonathani akamwambia Daudi, BWANA, Mungu wa Israeli, na awe shahidi; nitakapokuwa nimekwisha kumwuliza baba yangu, kama wakati huu kesho, au siku ya tatu, angalia, kama liko neno jema la kumfaa Daudi, je! Nisikupelekee habari na kukufunulia neno hili?
13. BWANA anitende mimi, Yonathani, hivyo, na kuzidi, ikiwa yampendeza babangu kukutenda mabaya, nisipokufunulia haya, na kukupeleka uende zako kwa amani; na BWANA awe pamoja nawe, kama alivyokuwa pamoja na baba yangu.
14. Nawe utanionyesha fadhili za BWANA, ili nisife, si wakati huu tu maadamu mimi ni hai;
15. lakini pamoja na hayo, hata jamaa yangu pia hutawaondolea kabisa fadhili zako; la, hata wakati ule BWANA atakapokuwa amewaondoa kabisa adui za Daudi wote pia katika uso wa nchi.
16. Basi Yonathani akafanya agano na jamaa yake Daudi, akisema, BWANA naye atayataka mkononi mwa adui zake Daudi.