18. Kisha Yonathani akamwambia, Kesho ni mwandamo wa mwezi, nawe utakosekana, kwa sababu kiti chako kitakuwa hakina mtu.
19. Nawe ukiisha kungoja siku tatu, shuka upesi ufike kuko huko ulikojificha, siku ya shughuli ile; nawe kaa karibu na kile kichuguu kule.
20. Nami nitapiga mishale mitatu kando-kando yake, kana kwamba ninapiga shabaha.
21. Kisha, angalia, nitamtuma mtoto na kumwambia, Nenda ukaitafute mishale. Hapo nikimwambia yule mtoto, Tazama, mishale iko upande wako huu, itwae; basi uje, maana iko amani kwako, wala hapana hatari, BWANA aishivyo.
22. Bali nikimwambia yule mtoto, Tazama, mishale iko huko mbele yako; basi enenda zako, kwa maana BWANA amekuamuru uende zako.
23. Na kwa habari ya neno lile tulilonena, wewe na mimi, angalia BWANA yu kati ya wewe na mimi milele.
24. Basi Daudi akajificha shambani; na mwezi ulipoandama, mfalme aliketi kula chakula.
25. Mfalme aliketi kitini mwake kama sikuzote, katika kiti kilichokuwa karibu na ukuta; Yonathani alikuwa mbele yake; Abneri naye akaketi karibu na Sauli; lakini mahali pake Daudi palikuwa hapana mtu.
26. Lakini Sauli hakusema neno siku ile; maana alidhani ya kuwa, Amepatikana na neno, hakutakata; hakosi yeye hakutakata.
27. Hata siku ya pili baada ya mwandamo wa mwezi, mahali pake palikuwa hapana mtu; basi Sauli akamwambia Yonathani mwanawe, Mbona mwana wa Yese haji kula chakula, jana wala leo?
28. Naye Yonathani akamjibu Sauli, Daudi alitaka sana nimpe ruhusa aende Bethlehemu;
29. akasema, Tafadhali nipe ruhusa niende; kwa maana jamaa yetu wana dhabihu mjini mwetu; na ndugu yangu ameniamuru niende; basi sasa, kama nimeona kibali machoni pako, nakuomba, niondoke; nikawatazame ndugu zangu. Ndiyo sababu hakuja mezani pa mfalme.
30. Basi hasira yake Sauli ikawaka juu ya Yonathani, akamwambia, Wewe, mwana wa mke mkaidi, asi, je! Mimi sijui ya kuwa umemchagua huyo mwana wa Yese, kwa aibu yako mwenyewe, na kwa aibu ya uchi wa mama yako.
31. Maana wakati mwana wa Yese akiwa hai juu ya nchi, wewe hutafanikiwa, wala ufalme wako. Basi, sasa peleka, ukamlete kwangu, maana hakika yake atakufa huyu.
32. Yonathani akamjibu Sauli, baba yake, akamwambia, Auawe kwa sababu gani? Amefanya nini?