1 Sam. 2:12-27 Swahili Union Version (SUV)

12. Basi, hao wana wa Eli walikuwa watu wasiofaa kitu; hawakumjali BWANA,

13. wala haki ya makuhani ilivyokuwa kwa watu. Wakati huo mtu ye yote alipotoa dhabihu wakati wo wote, ndipo huja mtumishi wa kuhani, nyama ilipokuwa katika kutokota, naye akawa na uma wa meno matatu mkononi mwake;

14. naye huutia kwa nguvu humo chunguni, au birikani, au sufuriani, au chomboni; nyama yote iliyoinuliwa kwa huo uma kuhani huichukua mwenyewe. Ndivyo walivyofanya huko Shilo kwa Waisraeli wote waliokuja huko.

15. Tena, kabla ya kuteketeza mafuta, huja mtumishi wa kuhani, akamwambia yule mwenye kuitoa dhabihu, Mtolee kuhani nyama ya kuoka; kwa kuwa hataki kupewa nyama iliyotokoswa, bali nyama mbichi.

16. Tena, ikiwa mtu yule amwambia, Hawakosi wataichoma moto hayo mafuta kwanza, kisha utwae kadiri roho yako itakavyopenda; ndipo husema, Sivyo, lakini sharti unipe sasa hivi; la, hunipi, basi nitaitwaa kwa nguvu.

17. Hivyo dhambi yao wale vijana ilikuwa kubwa sana machoni pa BWANA; kwa maana hao watu walidharau sadaka ya BWANA.

18. Lakini Samweli alikuwa akitumika mbele za BWANA, naye alikuwa kijana, mwenye kuvaa naivera ya kitani.

19. Tena mamaye humfanyizia kanzu ndogo, na kumletea mwaka kwa mwaka, hapo alipokwea pamoja na mumewe ili kutoa dhabihu kila mwaka.

20. Naye Eli akambariki Elkana na mkewe, akasema, BWANA na akupe uzao kwa mwanamke huyu, badala ya azimo aliloazimiwa BWANA. Kisha wakaenda nyumbani kwao.

21. Naye BWANA akamwangalia Hana, naye akachukua mimba, akazaa watoto, wa kiume watatu na wa kike wawili. Naye huyo mtoto Samweli akakua mbele za BWANA.

22. Basi Eli alikuwa mzee sana; naye alisikia habari za mambo yote ambayo wanawe waliwatenda Waisraeli; na jinsi walivyolala na wanawake waliokuwa wakitumika mlangoni pa hema ya kukutania.

23. Akawaambia, Mbona mnatenda mambo kama hayo? Maana nasikia habari za matendo yenu mabaya kwa watu hawa wote.

24. Sivyo hivyo, wanangu, kwa maana habari hii ninayoisikia si habari njema; mnawakosesha watu wa BWANA.

25. Mtu mmoja akimkosa mwenzake, Mungu atamhukumu; lakini mtu akimkosa BWANA, ni nani atakayemtetea? Lakini hawakuisikia sauti ya baba yao, kwa sababu BWANA amekusudia kuwaua.

26. Na yule mtoto, Samweli, akazidi kukua akapata kibali kwa BWANA, na kwa watu pia.

27. Kisha mtu wa Mungu akamwendea Eli, akamwambia, BWANA asema hivi, Je! Mimi sikujidhihirisha nafsi yangu kwa nyumba ya baba yako, walipokuwa katika Misri, wakiitumikia nyumba ya Farao?

1 Sam. 2