29. Naye Daudi akamjibu, Je! Mimi nimekosa nini sasa? Je! Si neno kubwa hilo?
30. Naye akamgeukia ili kumwelekea mtu mwingine, akasema naye jinsi ile ile; na watu wakamjibu tena jinsi ile ile kama ya kwanza.
31. Na maneno hayo aliyosema Daudi yaliposikiwa, watu wakamweleza Sauli; naye akatuma mtu kwenda kumwita.
32. Daudi akamwambia Sauli, Asizimie moyo mtu ye yote kwa ajili ya huyu; mimi mtumishi wako nitakwenda kupigana na Mfilisti huyu.
33. Sauli akamwambia Daudi, Huwezi wewe kumwendea Mfilisti huyu upigane naye; maana wewe u kijana tu; na huyu ni mtu wa vita tangu ujana wake.
34. Daudi akamwambia Sauli, Mtumishi wako alikuwa akichunga kondoo za baba yake, na alipokuwa akija simba, au dubu, akamkamata mwana-kondoo wa lile kundi,
35. mimi hutoka nikamfuata, nikampiga, nikampokonya kinywani mwake; na akinirukia, humshika ndevu zake, nikampiga, nikamwua.
36. Mtumishi wako alimwua simba na dubu pia; na huyu Mfilisti asiyetahiriwa atakuwa kama mmoja wao, kwa sababu amewatukana majeshi ya Mungu aliye hai.
37. Daudi akasema, BWANA aliyeniokoa na makucha ya simba, na makucha ya dubu, ataniokoa na mkono wa Mfilisti huyu. Sauli akamwambia Daudi, Enenda, na BWANA atakuwa pamoja nawe.
38. Ndipo Sauli akamvika Daudi mavazi yake ya vita, akamtia chapeo cha shaba kichwani, akamvika dirii.
39. Naye Daudi akajifunga upanga juu ya mavazi yake, akajaribu kwenda; maana alikuwa hajavijaribu. Daudi akamwambia Sauli, Siwezi kwenda na vitu hivi, maana sikuvijaribu. Basi Daudi akavivua.
40. Akaichukua fimbo yake mkononi, akajichagulia mawe laini matano katika kijito cha maji, akayatia katika mfuko wa kichungaji aliokuwa nao, maana ni mkoba wake, na kombeo lake alikuwa nalo mkononi mwake, akamkaribia yule Mfilisti.
41. Huyo Mfilisti naye akamsogelea Daudi na kumkaribia; na mtu yule aliyemchukulia ngao yake akamtangulia.