1 Sam. 14:41-52 Swahili Union Version (SUV)

41. Kwa hiyo Sauli akamwambia BWANA, Mungu wa Israeli, [Kwani usimjibu mtumishi wako leo? Ikiwa dhambi i ndani yangu, au ndani yake Yonathani mwanangu, Ee BWANA, Mungu wa Israeli, utoe Urimu; bali ukisema hivi, Dhambi i katika watu wako Israeli,] utoe Thumimu. Basi Yonathani na Sauli wakatwaliwa, lakini watu wakapona.

42. Basi Sauli akasema, Sasa piga kati ya mimi na mwanangu Yonathani, [naye awaye yote ambaye BWANA atamtwaa, atakufa. Nao watu wakamwambia Sauli, La! Sivyo hivyo; lakini Sauli akawaweza watu. Nao wakapiga kati ya yeye na mwanawe Yonathani,] naye Yonathani akatwaliwa.

43. Ndipo Sauli akamwambia Yonathani, Niambie ulilolifanya. Basi Yonathani akamwambia, akasema, Ni kweli, mimi nalionja asali kidogo kwa ncha ya fimbo ile iliyokuwa mkononi mwangu; na tazama, imenipasa kufa.

44. Naye Sauli akasema, Mungu anifanyie hivi, na kuzidi; kwa kuwa hakika utakufa, Yonathani.

45. Walakini watu wakamwambia Sauli, Je! Atakufa Yonathani, ambaye ndiye aliyeufanya huo wokovu mkuu katika Israeli? Hasha! Aishivyo BWANA, hautaanguka chini hata unywele mmoja wa kichwa chake; kwa maana ametenda kazi pamoja na Mungu leo. Hivyo hao watu wakamponya Yonathani, asife.

46. Ndipo Sauli akakwea kuacha kuwafuata Wafilisti; nao Wafilisti wakaenda zao kwao.

47. Basi Sauli alipokwisha kuutwaa ufalme juu ya Israeli, alipigana na adui zake zote pande zote, juu ya Moabu, na juu ya wana wa Amoni, na juu ya Edomu, na juu ya wafalme wa Soba, na juu ya Wafilisti; na po pote alipogeukia, akawashinda.

48. Naye akatenda kwa ushujaa, akawapiga Waamaleki, na kuwaokoa Waisraeli katika mikono yao waliowateka nyara.

49. Basi, wana wa Sauli walikuwa ni hawa, Yonathani, na Ishvi, na Malkishua; na majina ya binti zake wawili yalikuwa haya; jina lake wa kwanza aliitwa Merabu, na jina lake mdogo aliitwa Mikali;

50. na jina lake mkewe Sauli aliitwa Ahinoamu, binti Ahimaasi. Tena, jina la jemadari wa jeshi lake aliitwa Abneri, mwana wa Neri, aliyekuwa baba mdogo wa Sauli.

51. Na Kishi, babaye Sauli, na Neri, babaye Abneri, walikuwa wana wa Abieli.

52. Tena, kulikuwa na vita vikali sana juu ya Wafilisti siku zote za Sauli, naye Sauli alipomwona mtu ye yote aliyekuwa hodari, au mtu ye yote aliyekuwa shujaa, humtwaa ili awe pamoja naye.

1 Sam. 14