1 Sam. 14:33-40 Swahili Union Version (SUV)

33. Ndipo wakamwambia Sauli, wakisema, Angalia, watu hao wanakosa juu ya BWANA, kwa jinsi wanavyokula pamoja na damu. Naye akasema, Ninyi mmefanya kwa hiana; vingirisheni kwangu leo jiwe kubwa.

34. Kisha Sauli akasema, Haya! Tawanyikeni katikati ya watu mkawaambie, Nileteeni hapa kila mtu ng’ombe wake, na kila mtu kondoo wake, mkawachinje hapa na kula; wala msikose juu ya BWANA, kwa kula pamoja na damu. Nao watu wote wakaleta kila mtu ng’ombe wake pamoja naye usiku ule, nao wakawachinja hapo.

35. Naye Sauli akamjengea BWANA madhabahu; hiyo ndiyo madhabahu ya kwanza aliyomjengea BWANA.

36. Kisha Sauli akasema, Haya! Na tushuke kuwafuata Wafilisti wakati wa usiku, na kuwateka nyara hata mapambazuko, wala tusiwaache hata mmoja wao. Nao wakamjibu, Fanya yo yote uyaonayo kuwa ni mema. Ndipo yule kuhani akasema, Na tumkaribie Mungu hapa.

37. Basi Sauli akataka shauri kwa Mungu, Je! Nishuke ili kuwafuatia Wafilisti? Je! Utawatia mikononi mwa Israeli? Lakini hakumjibu neno lo lote siku ile.

38. Ndipo Sauli akasema, Karibieni hapa, enyi wakuu wote wa watu; mjue na kuona dhambi hii ya leo imekuwa katika kosa gani.

39. Kwa maana, aishivyo BWANA, awaokoaye Israeli, ijapokuwa i katika Yonathani, mwanangu, kufa atakufa. Lakini miongoni mwa watu wote hakuna mtu ye yote aliyemjibu.

40. Ndipo akawaambia Israeli wote, Ninyi mtakuwa upande mmoja, na mimi na mwanangu Yonathani tutakuwa upande wa pili. Basi wakamwambia Sauli, Fanya uonayo kuwa ni mema.

1 Sam. 14