1. Kisha Samweli akawaambia Israeli wote, Angalieni, nimeisikiliza sauti yenu katika hayo yote mliyoniambia, nami nimemtawaza mfalme juu yenu.
2. Basi sasa, angalieni, mfalme anakwenda mbele yenu; na mimi ni mzee, mwenye mvi; tena, tazameni, wana wangu wapo pamoja nanyi; nami nimekwenda mbele yenu toka ujana wangu hata leo.
3. Nami nipo hapa; basi, mnishuhudie mbele za BWANA, na mbele ya masihi wake, nalitwaa ng’ombe wa nani? Au nalitwaa punda wa nani? Au ni nani niliyemdhulumu? Ni nani niliyemwonea? Au kwa mkono wa nani nimepokea rushwa inipofushe macho? Nami nitawarudishia ninyi.
4. Nao wakasema, hukutudhulumu, wala hukutuonea, wala hukupokea kitu kwa mkono wa mtu awaye yote.
5. Akawaambia, BWANA ni shahidi juu yenu, na masihi wake ni shahidi leo, ya kuwa hamkuona kitu mkononi mwangu. Nao wakasema, Yeye ni shahidi.
6. Samweli akawaambia watu, Ni yeye BWANA aliyewaweka Musa na Haruni, ndiye yeye aliyewatoa baba zenu kutoka nchi ya Misri.
7. Basi sasa simameni, ili niwahutubie mbele za BWANA, kwa kutaja matendo yote ya haki ya BWANA, aliyowatendea ninyi na baba zenu.
8. Yakobo alipokuwa ameingia Misri, na baba zenu walipomlilia BWANA, ndipo BWANA akawapeleka Musa na Haruni, nao wakawatoa baba zenu kutoka Misri, wakawakalisha mahali hapa.
9. Lakini wakamsahau BWANA, Mungu wao, naye akawauza na kuwatia katika mikono ya Sisera, jemadari wa jeshi la Hazori, na katika mikono ya Wafilisti, na katika mikono ya mfalme wa Moabu, nao wakapigana nao.