18. Naye akasema, Mjakazi wako na aone kibali machoni pako. Basi huyo mwanamke akaenda zake, naye akala chakula, wala uso wake haukukunjamana tena.
19. Wakaondoka asubuhi na mapema, wakasali mbele za BWANA, kisha wakarejea na kufika nyumbani kwao huko Rama; Elkana akamjua mkewe Hana; naye BWANA akamkumbuka.
20. Ikawa, wakati ulipowadia, Hana akachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; akamwita jina lake Samweli, akisema, Kwa kuwa nimemwomba kwa BWANA.
21. Kisha yule mtu, Elkana, na watu wote wa nyumbani mwake, wakakwea kwenda kumtolea BWANA dhabihu ya mwaka, na nadhiri yake.
22. Bali Hana hakukwea; maana alimwambia mumewe, Sitakwea mimi hata mtoto wangu atakapoachishwa maziwa, hapo ndipo nitakapomleta, ili ahudhurie mbele za BWANA, akae huko daima.
23. Elkana, mumewe, akamwambia, Haya, fanya uonavyo vema; ngoja hata utakapomwachisha maziwa; BWANA na alithibitishe neno lake tu. Basi yule mwanamke akangoja, akamnyonyesha mtoto wake, hata akamwachisha maziwa.
24. Naye alipokuwa amekwisha kumwachisha maziwa, akamchukua pamoja naye, na ng’ombe watatu, na efa moja ya unga, na chupa ya divai, akamleta nyumbani kwa BWANA, huko Shilo; na yule mtoto alikuwa mtoto mdogo.
25. Nao wakamchinja huyo ng’ombe, wakamleta mtoto kwa Eli.
26. Akasema, Ee bwana wangu, kama iishivyo roho yako, bwana wangu, mimi ndimi yule mwanamke aliyesimama karibu nawe hapa, nikimwomba BWANA.
27. Naliomba nipewe mtoto huyu; BWANA akanipa dua yangu niliyomwomba;