1. Ikawa baada ya hayo, Nahashi, mfalme wa wana wa Amoni, akafa, akamiliki mwanawe mahali pake.
2. Naye Daudi akasema, Nitamtendea wema Hanuni, mwana wa Nahashi, kwa kuwa babaye alinitendea mimi wema. Basi Daudi akapeleka wajumbe ili kumtuliza kwa habari za babaye. Wakaja watumishi wa Daudi katika nchi ya wana wa Amoni kwa Hanuni, ili wamtulize.
3. Lakini wakuu wa wana wa Amoni wakamwambia Hanuni, Je! Waona Daudi amheshimu babayo kwa kukupelekea wafariji? Je! Hawakukujia watumishi wake ili kuiangalia nchi, na kuiangamiza, na kuipeleleza?
4. Basi Hanuni akawatwaa watumishi wa Daudi, akawanyoa, akawakatia nguo zao katikati, hata matakoni, akawatoa waende zao.
5. Wakaenda watu wakamwambia Daudi jinsi walivyotendewa wale watu. Naye akatuma watu kuwalaki; kwa sababu watu hao walikuwa wametahayarika sana. Mfalme akasema, Ngojeni Yeriko, hata mtakapoota ndevu zenu, ndipo mrudi.
6. Na wana wa Amoni walipoona ya kuwa wamekuwa machukizo kwa Daudi, Hanuni na wana wa Amoni wakapeleka talanta elfu za fedha ili kujiajiria magari na wapanda farasi kutoka Mesopotamia, na kutoka Atam-maaka, na kutoka Soba.
7. Basi wakajiajiria magari thelathini na mbili elfu, na mfalme wa Maaka na watu wake; nao walikuja wakatua mbele ya Medeba. Na wana wa Amoni wakakusanyika kutoka miji yao, wakaja vitani.
8. Basi Daudi aliposikia habari akamtuma Yoabu, na jeshi lote la mashujaa.