1 Nya. 16:24-40 Swahili Union Version (SUV)

24. Wahubirini mataifa habari za utukufu wake,Na watu wote habari za maajabu yake.

25. Kwa kuwa BWANA ni mkuu mwenye kusifiwa sana;Na wa kuhofiwa kuliko miungu yote.

26. Maana miungu yote ya watu si kitu;Lakini BWANA ndiye aliyezifanya mbingu.

27. Heshima na adhama ziko mbele zake;Nguvu na furaha zipo mahali pake.

28. Mpeni BWANA, enyi jamaa za watu,Mpeni BWANA utukufu na nguvu.

29. Mpeni BWANA utukufu wa jina lake;Leteni sadaka, mje mbele zake;Mwabuduni BWANA kwa uzuri wa utakatifu;

30. Tetemekeni mbele zake, nchi yote.Naam, ulimwengu umethibitika usitikisike;

31. Mbingu na zifurahi, nchi na ishangilie;Na waseme katika mataifa, BWANA ametamalaki;

32. Bahari na ivume na vyote viijazavyo;Mashamba na yashangilie na vyote vilivyomo;

33. Ndipo miti yote ya mwituni iimbe kwa furaha,Mbele za BWANA,Kwa maana anakuja aihukumu nchi.

34. Mshukuruni BWANA kwa kuwa ni mwema;Kwa maana fadhili zake ni za milele.

35. Nanyi mkaseme,Ee Mungu wa wokovu wetu, utuokoe,Utukusanye kwa kututoa katika mataifa,Tulishukuru jina lako takatifu,Tuzifanyie shangwe sifa zako.

36. Na ahimidiwe BWANA, Mungu wa Israeli, tangu milele hata milele. Na watu wote wakasema, Amina; wakamhimidi BWANA.

37. Basi akawaacha huko, mbele ya sanduku la agano la BWANA, Asafu na nduguze, ili watumike mbele ya sanduku daima, kila siku kama ilivyokuwa kazi yake.

38. Naye Obed-edomu, pamoja na ndugu zao, sitini na wanane; Obed-edomu na mwana wa Yeduthuni, na Hosa, wawe mabawabu;

39. na Sadoki kuhani, na nduguze makuhani, mbele ya maskani ya BWANA katika mahali pa juu palipokuwa huko Gibeoni,

40. ili kumtolea BWANA sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa daima asubuhi na jioni, naam, sawasawa na yote yaliyoandikwa katika torati ya BWANA, aliyowaamuru Israeli;

1 Nya. 16