5. Na hao wenyeji wa Yebusi wakamwambia Daudi, Hutaingia humu. Walakini Daudi akaitwaa ngome ya Sayuni; huu ndio mji wa Daudi.
6. Naye Daudi akasema, Mtu ye yote atakayekuwa wa kwanza wa kuwapiga Wayebusi, yeye atakuwa mkuu na jemadari. Naye wa kwanza aliyepanda ni Yoabu mwana wa Seruya, naye akawa mkuu.
7. Basi Daudi akakaa ngomeni; kwa hiyo huuita mji wa Daudi.
8. Akaujenga huo mji pande zote, toka Milo na kuuzunguka; naye Yoabu akautengeneza mji uliosalia.
9. Naye Daudi akaendelea, akazidi kuwa mkuu; kwa maana BWANA wa majeshi alikuwa pamoja naye.
10. Basi hawa ndio wakuu wa mashujaa aliokuwa nao Daudi, waliojitia nguvu pamoja naye katika ufalme wake, pamoja na Israeli wote, ili kumfanya awe mfalme, sawasawa na neno la BWANA alilonena juu ya Israeli.
11. Na hii ndiyo hesabu ya hao mashujaa aliokuwa nao Daudi; Yashobeamu, Mhakmoni, mkuu wa maakida; huyo aliuinua mkuki wake juu ya watu mia tatu, akawaua pamoja.
12. Na baada yake kulikuwa na Eleazari, mwana wa Dodai, Mwahohi, mmojawapo wa wale mashujaa watatu.
13. Huyo alikuwa pamoja na Daudi huko Pasdamimu; ndiko Wafilisti walikokusanyika vitani, palipokuwa na konde limejaa shayiri; na hao watu wakakimbia mbele ya Wafilisti.
14. Ndipo hao wakasimama katikati ya konde lile, wakalipigania, wakawaua Wafilisti; naye BWANA akafanya wokovu mkuu.
15. Tena, watatu miongoni mwa wale thelathini waliokuwa wakuu wakashuka mwambani, wakamwendea Daudi, hata pango la Adulamu; na jeshi la Wafilisti walikuwa wamefanya kambi bondeni mwa Warefai.
16. Na Daudi wakati ule alikuwako ngomeni, na walinzi wa Wafilisti wakati ule walikuwa huko Bethlehemu.