1 Kor. 9:15-23 Swahili Union Version (SUV)

15. Lakini mimi sikutumia mambo hayo hata moja. Wala siyaandiki hayo ili iwe hivyo kwangu mimi; maana ni heri nife kuliko mtu awaye yote abatilishe huku kujisifu kwangu.

16. Maana, ijapokuwa naihubiri Injili, sina la kujisifia; maana nimewekewa sharti; tena ole wangu nisipoihubiri Injili!

17. Maana nikiitenda kazi hii kwa hiari yangu nina thawabu; ila ikiwa si kwa hiari yangu, nimeaminiwa uwakili.

18. Basi thawabu yangu ni nini? Ni hii, ya kuwa nihubiripo, nitaitoa Injili bila gharama, bila kutumia kwa utimilifu uwezo wangu nilio nao katika Injili.

19. Maana, ingawa nimekuwa huru kwa watu wote, nalijifanya mtumwa wa wote, ili nipate watu wengi zaidi.

20. Nalikuwa kama Myahudi kwa Wayahudi, ili niwapate Wayahudi; kwa wale walio chini ya sheria, nalikuwa kama chini ya sheria, (ingawa mimi mwenyewe si chini ya sheria), ili niwapate walio chini ya sheria.

21. Kwa wale wasio na sheria nalikuwa kama sina sheria, (si kwamba sina sheria mbele za Mungu, bali mwenye sheria mbele za Kristo), ili niwapate hao wasio na sheria.

22. Kwa wanyonge nalikuwa mnyonge, ili niwapate wanyonge. Nimekuwa hali zote kwa watu wote, ili kwa njia zote nipate kuwaokoa watu.

23. Nami nafanya mambo yote kwa ajili ya Injili ili kuishiriki pamoja na wengine.

1 Kor. 9