1 Kor. 11:8-27 Swahili Union Version (SUV)

8. Maana mwanamume hakutoka katika mwanamke, bali mwanamke katika mwanamume.

9. Wala mwanamume hakuumbwa kwa ajili ya mwanamke, bali mwanamke kwa ajili ya mwanamume.

10. Kwa hiyo imempasa mwanamke awe na dalili ya kumilikiwa kichwani, kwa ajili ya malaika.

11. Walakini si mwanamke pasipo mwanamume, wala mwanamume pasipo mwanamke, katika Bwana.

12. Maana kama mwanamke alitoka katika mwanamume, vile vile mwanamume naye huzaliwa na mwanamke; na vitu vyote asili yake hutoka kwa Mungu. Hukumuni ninyi wenyewe katika nafsi zenu.

13. Je! Inapendeza mwanamke amwombe Mungu asipofunikwa kichwa?

14. Je! Hayo maumbile yenyewe hayawafundishi ya kwamba mwanamume akiwa na nywele ndefu ni aibu kwake?

15. Lakini mwanamke akiwa na nywele ndefu ni fahari kwake. Kwa sababu amepewa zile nywele ndefu ili ziwe badala ya mavazi.

16. Lakini mtu ye yote akitaka kuleta fitina, sisi hatuna desturi kama hiyo, wala makanisa ya Mungu.

17. Lakini katika kuagiza haya, siwasifu, ya kwamba mnakusanyika, si kwa faida bali kwa hasara.

18. Kwa maana kwanza mkutanikapo kanisani nasikia kuna faraka kwenu; nami nusu nasadiki;

19. kwa maana lazima kuwapo na uzushi kwenu, ili waliokubaliwa wawe dhahiri kwenu.

20. Basi mkutanikapo pamoja haiwezekani kula chakula cha Bwana;

21. kwa maana kila mmoja hutangulia kutwaa chakula chake katika kule kula; hata huyu ana njaa, na huyu amelewa.

22. Je! Hamna nyumba za kulia na kunywea? Au mnalidharau kanisa la Mungu, na kuwatahayarisha hao wasio na kitu? Niwaambieni? Niwasifu? La! Siwasifu kwa ajili ya hayo.

23. Kwa maana mimi nalipokea kwa Bwana niliyowapa nanyi, ya kuwa Bwana Yesu usiku ule aliotolewa alitwaa mkate,

24. naye akiisha kushukuru akaumega, akasema, Huu ndio mwili wangu ulio kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu.

25. Na vivi hivi baada ya kula akakitwaa kikombe, akisema, Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu; fanyeni hivi kila mnywapo, kwa ukumbusho wangu.

26. Maana kila mwulapo mkate huu na kukinywea kikombe hiki, mwaitangaza mauti ya Bwana hata ajapo.

27. Basi kila aulaye mkate huo, au kukinywea kikombe hicho cha Bwana isivyostahili, atakuwa amejipatia hatia ya mwili na damu ya Bwana.

1 Kor. 11