45. basi, uyasikie huko mbinguni maombi yao na dua yao, ukaitetee haki yao.
46. Ikiwa wamekutenda dhambi, (maana hakuna mtu asiyetenda dhambi), hata ukawaghadhibikia, ukawatia katika mikono ya adui zao, wawachukue mateka mpaka nchi ya adui zao, iliyo mbali au iliyo karibu;
47. basi, wakijirudia nafsi zao katika nchi ile watakayochukuliwa mateka, wakitubu, na kukusihi katika nchi ya hao waliowachukua mateka, wakisema, Tumekosa, tumefanya ukaidi, tumetenda maovu;
48. watakaporejea kwako kwa mioyo yao yote, na kwa nia zao zote, katika nchi ya adui zao, waliowachukua mateka, wakikuomba, kwa kuikabili nchi yao, uliyowapa baba zao, na mji huu uliouchagua, na nyumba hii niliyoijenga kwa jina lako;
49. basi, uyasikie maombi yao na dua yao, huko mbinguni, makao yako, ukaitetee haki yao;
50. ukawasamehe watu wako waliokutenda dhambi, na makosa yao yote waliyokukosa; ukawape kuonewa huruma mbele yao waliowachukua mateka, ili wapate kuwahurumia.
51. Kwa kuwa ni watu wako, na urithi wako, uliowatoa katika Misri, toka katikati ya tanuu ya chuma.
52. Macho yako na yafumbuke, na kuielekea dua ya mtumwa wako, na dua za watu wako Israeli, ukawasikilize kila wakati watakapokulilia.
53. Kwa maana uliwatenga na watu wote wa dunia, wawe urithi wako, kama ulivyonena kwa mdomo wa Musa, mtumishi wako, hapo ulipowatoa baba zetu katika Misri, Ee Bwana MUNGU.
54. Hata ikawa, Sulemani alipokwisha kumwomba BWANA maombi hayo, na dua hiyo yote, akasimama na kuondoka hapo mbele ya madhabahu ya BWANA, hapo alipokuwa amepiga magoti, na kuikunjua mikono yake kuelekea mbinguni.
55. Akasimama, na kuwabariki mkutano wote wa Israeli kwa sauti kuu, akasema,
56. Na ahimidiwe BWANA, aliyewapa watu wake Israeli kustarehe, vile vile kama yote aliyoyaahidi. Halikukosa kupatikana neno lo lote katika ahadi yake njema, aliyoahidi kwa mkono wa Musa, mtumishi wake.
57. BWANA, Mungu wetu, na akae nasi, kama alivyokaa na baba zetu; asituache, wala asitutupe;
58. aielekeze mioyo yetu kwake, ili tuende katika njia zake zote, na kuzishika amri zake, na sheria zake, na hukumu zake, alizowaamuru baba zetu.