1 Fal. 7:17-30 Swahili Union Version (SUV)

17. Kulikuwa na nyavu kama kazi ya kusuka, na masongo ya mikufu, kwa taji zilizokuwako juu ya vichwa vya nguzo; saba kwa taji moja, na saba kwa taji ya pili

18. Hivyo akazifanya nguzo; na kulikuwa na safu mbili za kuzunguka juu ya wavu mmoja, zifunike taji zilizokuwako juu ya vichwa vya nguzo; akafanya vivyo hivyo kwa taji ya pili.

19. Na taji zilizokuwa juu ya nguzo ukumbini zilikuwa za kazi ya mayungi, mikono minne.

20. Kulikuwako tena taji juu ya nguzo mbili, karibu na uvimbe uliokuwako kando ya wavu; na makomamanga yalikuwa mia mbili, safu safu pande zote juu ya taji ya pili.

21. Akazisimamisha nguzo ukumbini pa hekalu; akaisimamisha nguzo ya kuume, akaiita jina lake Yakini; akaisimamisha nguzo ya kushoto, akaiita jina lake Boazi.

22. Na juu ya nguzo kulikuwa na kazi ya mayungi; hivyo mambo ya nguzo yakatimia.

23. Tena akaifanya bahari ya kusubu, mikono kumi toka ukingo hata ukingo, ikaviringana, na mikono mitano ilikuwa kwenda juu kwake; na uzi wa mikono thelathini kuizunguka kabisa.

24. Na chini ya ukingo wake kulikuwa na maboga yaliyoizunguka, kwa mikono kumi, yakiizunguka bahari; kulikuwa na safu mbili za hayo maboga, yakafanywa kalibuni hapo bahari ilipofanywa.

25. Ikakaa juu ya ng’ombe kumi na wawili, watatu wakitazama kaskazini, na watatu wakitazama magharibi, na watatu wakitazama kusini, na watatu wakitazama mashariki; na bahari iliwekwa juu yao, na pande zao za nyuma zote zilikuwa ndani.

26. Na unene wake ulikuwa nyanda nne; na ukingo wake ukafanywa kama ukingo wa kikombe, kama ua la yungi; huingia bathi elfu mbili.

27. Akayafanya yale matako kumi ya shaba; mikono minne urefu wa tako moja, na mikono minne upana wake, na mikono mitatu kwenda juu kwake.

28. Na kazi ya matako ndiyo hii; yalikuwa na papi; na papi zilikuwa katikati ya vipandio;

29. na juu ya papi zilizokuwa katikati ya vipandio kulikuwa na simba, na ng’ombe, na makerubi; na juu ya vipandio kulikuwa na tako; na chini ya simba na ng’ombe kulikuwa na masongo ya kazi ya kupembeza.

30. Kila tako lilikuwa na magurudumu manne ya shaba, na vipini vya shaba; na miguu yake minne ilikuwa na mataruma; chini ya birika yalikuwako mataruma ya kusubu, yenye masongo kila moja mbavuni.

1 Fal. 7