1 Fal. 7:1-17 Swahili Union Version (SUV)

1. Naye Sulemani alikuwa katika kuijenga nyumba yake mwenyewe miaka kumi na mitatu, akaimaliza nyumba yake yote.

2. Kwa kuwa aliijenga nyumba ya mwitu wa Lebanoni; mikono mia urefu wake, na mikono hamsini upana wake, na mikono thelathini kwenda juu kwake, juu ya safu nne za nguzo za mwerezi, na mihimili ya mwerezi juu ya nguzo.

3. Ikafunikwa juu kwa mwerezi juu ya mihimili arobaini na mitano, iliyokuwa juu ya nguzo; kumi na mitano kwa safu.

4. Na madirisha yalikuwako safu tatu, mwangaza kuelekea mwangaza katika madaraja matatu.

5. Na milango yote na miimo ilikuwa ya mraba, ilivyoangaziwa; na mwangaza kuelekea mwangaza katika madaraja matatu.

6. Akaifanya baraza ya nguzo; mikono hamsini urefu wake, na mikono thelathini upana wake; na ukumbi mbele yake; na nguzo na mihimili minene mbele yake.

7. Akaifanya baraza ya kiti cha enzi, ili ahukumu ndani yake, ndiyo baraza ya hukumu; nayo ikafunikwa mwerezi tangu sakafu mpaka dari.

8. Nayo nyumba yake atakayokalia, katika behewa nyingine iliyokuwa ndani kupita baraza, ilikuwa ya kazi kama hiyo. Tena akamjengea nyumba binti Farao, (ambaye Sulemani alikuwa amemwoa), mfano wa ile baraza.

9. Hizi zote zilikuwa za mawe ya thamani, mawe ya kuchongwa, sawasawa na cheo, yaliyokatwa kwa misumeno, ndani na nje, tangu msingi hata mawe ya juu, na nje vile vile hata behewa kuu.

10. Nao msingi ulikuwa wa mawe ya thamani, mawe makubwa, mawe mikono kumi, na mawe ya mikono minane.

11. Na juu kulikuwa na mawe ya thamani, mawe ya kuchongwa, sawasawa na cheo, na mierezi.

12. Na behewa kubwa pande zote ilikuwa na safu tatu za mawe ya kuchongwa, na safu moja ya mihimili ya mierezi; mfano wa behewa ya ndani ya nyumba ya BWANA, na ukumbi wa nyumba.

13. Mfalme Sulemani akatuma watu kumleta Huramu kutoka Tiro.

14. Naye alikuwa mwana wa mwanamke mjane wa kabila ya Naftali, na babaye alikuwa mtu wa Tiro, mfua shaba; naye alikuwa mwingi wa hekima na akili, mstadi wa kufanya kazi zote za shaba. Akamfikilia mfalme Sulemani, akamfanyia kazi yake yote.

15. Kwa maana alizifanyiza zile nguzo mbili za shaba, mikono kumi na minane kwenda juu kwake kila moja; na uzi wa mikono kumi na miwili kuizunguka nguzo hii au hii.

16. Akafanya taji mbili za shaba iliyoyeyushwa za kuwekwa juu ya vichwa vya nguzo; kwenda juu kwake taji moja mikono mitano, na mikono mitano kwenda juu kwake taji ya pili.

17. Kulikuwa na nyavu kama kazi ya kusuka, na masongo ya mikufu, kwa taji zilizokuwako juu ya vichwa vya nguzo; saba kwa taji moja, na saba kwa taji ya pili

1 Fal. 7