29. Akaambiwa mfalme Sulemani ya kwamba, Yoabu amekimbilia Hemani kwa BWANA, naye, tazama, yuko madhabahuni. Ndipo Sulemani akamtuma Benaya, mwana wa Yehoyada, akisema, Enenda, umpige.
30. Basi Benaya akaja Hemani kwa BWANA, akamwambia, Mfalme asema hivi, Njoo utoke. Naye akajibu, La, sivyo; ila nitakufa papa hapa. Naye Benaya akamletea mfalme habari, akisema, Hivi ndivyo alivyonena Yoabu, na ndivyo alivyonijibu.
31. Mfalme akamwambia, Fanya alivyonena, umpige, ukamzike; ili uniondolee mimi na nyumba ya babangu damu aliyoimwaga Yoabu bure.
32. Naye BWANA atamrudishia damu yake kichwani pake mwenyewe, kwa kuwa aliwapiga watu wawili wenye haki, na wema kuliko yeye, akawaua kwa upanga, wala babangu Daudi hakujua habari hiyo; yaani Abneri, mwana wa Neri, jemadari wa jeshi la Israeli, na Amasa, mwana wa Yetheri, jemadari wa jeshi la Yuda.
33. Hivyo damu yao itarudi kichwani pa Yoabu, na kichwani pa wazao wake hata milele; ila kwa Daudi, na kwa wazao wake, na kwa nyumba yake, na kwa kiti chake cha enzi, kutakuwa na amani hata milele kutoka kwa BWANA.
34. Ndipo Benaya, mwana wa Yehoyada, akapanda, akampiga, akamwua; naye akazikwa katika nyumba yake mwenyewe iliyoko nyikani.
35. Kisha mfalme akamweka Benaya, mwana wa Yehoyada, mahali pake juu ya jeshi; na Sadoki, kuhani, mfalme akamweka mahali pa Abiathari.
36. Tena, mfalme akatuma watu akamwita Shimei, akamwambia, Ujijengee nyumba humu Yerusalemu, ukae ndani yake, wala usitoke humo kwenda mahali po pote.
37. Kwa kuwa siku ile ya kutoka kwako, na kuvuka kijito Kidroni, ujue hakika ya kwamba kufa utakufa; damu yako itakuwa juu ya kichwa chako mwenyewe.
38. Naye Shimei akamwambia mfalme, Neno hili ni jema; kama alivyosema bwana wangu mfalme, ndivyo atakavyofanya mtumwa wako. Basi Shimei akakaa Yerusalemu siku nyingi.
39. Ikawa miaka mitatu ilipokwisha, watumwa wawili wa Shimei wakatoroka kwenda kwa Akishi, mwana wa Maaka, mfalme wa Gathi. Wakamwambia Shimei, wakasema, Angalia, watumwa wako wako huko Gathi.
40. Shimei akaondoka, akatandika punda wake, akaenda Gathi kwa Akishi, ili kuwatafuta watumwa wake. Akaenda Shimei, akawaleta watumwa wake toka Gathi.
41. Naye Sulemani akaambiwa, ya kwamba Shimei alikuwa ametoka Yerusalemu kwenda Gathi, na kurudi tena.
42. Basi, mfalme akatuma watu, akamwita Shimei, akamwambia, Je! Sikukuapisha kwa BWANA, na kukushuhudia, kusema, Siku ile ya kutoka kwako ukienda mahali po pote, ujue hakika ya kwamba kufa utakufa? Nawe ukaniambia, Neno hili nililolisikia ni jema?
43. Mbona basi hukukishika kiapo cha BWANA, na amri niliyokuagiza?
44. Tena, mfalme akamwambia Shimei, Umejua uovu wote uliouona moyoni mwako, uliomtenda Daudi baba yangu; basi kwa hiyo BWANA atakurudishia uovu wako kichwani pako mwenyewe.
45. Ila mfalme Sulemani atakuwa amebarikiwa, na kiti cha enzi cha Daudi kitathibitika mbele za BWANA hata milele.
46. Basi mfalme akamwamuru Benaya, mwana wa Yehoyada; naye akatoka, akampiga, hata akafa. Nao ufalme ukawa imara mkononi mwa Sulemani.