11. Nawe sasa wasema, Enenda, umwambie bwana wako, Tazama, Eliya yupo.
12. Na itakuwa, mara mimi nikiondoka kwako, roho ya BWANA atakuchukua uende nisikojua; nami nitakapokwenda kumwambia Ahabu, naye asipokuona, ataniua, lakini mimi mtumishi wako namcha BWANA tangu ujana wangu.
13. Je! Bwana wangu hakuambiwa nilivyofanya hapo Yezebeli alipowaua manabii wa BWANA? Jinsi nilivyowaficha manabii wa BWANA, watu mia, hamsini hamsini katika pango, nikawalisha chakula na kuwapa maji?
14. Nawe sasa wasema, Enenda umwambie bwana wako, Tazama, Eliya yupo; basi, ataniua.
15. Eliya akasema, Kama BWANA wa majeshi aishivyo ambaye ninasimama mbele zake, hakika nitajionyesha kwake leo.
16. Basi, Obadia akaenda zake amwone Ahabu, akamwambia; naye Ahabu akaenda kumlaki Eliya.
17. Ikawa, Ahabu alipomwona Eliya, Ahabu akamwambia, Je! Ni wewe, Ewe mtaabishaji wa Israeli?
18. Naye akajibu, Si mimi niliyewataabisha Israeli; bali ni wewe, na nyumba ya baba yako, kwa kuwa mmeziacha amri za BWANA; nawe umewafuata mabaali.
19. Basi sasa upeleke watu, unikusanyie jamii ya Israeli katika mlima wa Karmeli, na wale manabii wa Baali mia nne na hamsini, na wale manabii wa Ashera mia nne, walao chakula mezani pa Yezebeli.
20. Basi, Ahabu akapeleka watu kwa wana wa Israeli wote, akawakusanya manabii pamoja katika mlima wa Karmeli.
21. Naye Eliya akawakaribia watu wote, akanena, Mtasita-sita katikati ya mawazo mawili hata lini? BWANA akiwa ndiye Mungu, mfuateni; bali ikiwa Baali ni Mungu, haya! Mfuateni yeye. Wale watu hawakumjibu neno.