1. Rehoboamu akaenda Shekemu; maana Israeli wote walikuwa wamekwenda Shekemu, ili kumfanya mfalme.
2. Ikawa Yeroboamu mwana wa Nebati alipopata habari (maana alikuwa akaliko Misri, huko alikokimbilia awe mbali na mfalme Sulemani; Yeroboamu akakaa huko Misri,
3. wakapeleka watu kwenda kumwita); basi Yeroboamu na jamii yote ya Israeli wakaenda, wakamwambia Rehoboamu, wakasema,
4. Baba yako alilifanya zito kongwa letu; basi sasa utupunguzie utumwa mzito tuliotumikishwa na baba yako, na lile kongwa zito alilotutwika, nasi tutakutumikia.
5. Akawaambia, Enendeni zenu hata siku ya tatu, kisha mnirudie tena. Watu wakaenda zao.
6. Mfalme Rehoboamu akataka shauri kwa wazee waliokuwa wakisimama mbele ya Sulemani, baba yake, alipokuwa hai, akasema, Mwanipa shauri gani ili niwajibu watu hawa?
7. Wakamwambia wakasema, Ukikubali kuwa mtumishi wa watu hawa leo, na kuwatumikia, na kuwajibu, na kuwapa maneno mazuri, basi watakuwa watumishi wako daima.