9. Basi BWANA akamghadhibikia Sulemani kwa sababu moyo wake umegeuka, naye amemwacha BWANA, Mungu wa Israeli, aliyemtokea mara mbili,
10. akamwamuru katika habari ya jambo lilo hilo asifuate miungu mingine; lakini yeye hakuyashika aliyoyaamuru BWANA.
11. Kwa hiyo BWANA akamwambia Sulemani, Kwa kuwa umefanya hayo, wala hukuyashika maagano yangu, na sheria zangu nilizokuamuru, hakika nitaurarua ufalme usiwe wako, nami nitampa mtumishi wako.
12. Walakini katika siku zako sitafanya haya, kwa ajili ya Daudi baba yako; nitaurarua utoke katika mkono wa mwana wako.
13. Lakini sitauondoa ufalme wote pia; nitampa mwana wako kabila moja, kwa ajili ya Daudi mtumishi wangu, na kwa ajili ya Yerusalemu niliouchagua.
14. Ndipo BWANA akamwondokeshea Sulemani adui, Hadadi Mwedomi; yeye alikuwa wa wazao wake mfalme wa Edomu.
15. Kwa maana ikawa, Daudi alipokuwako Edomu, naye Yoabu, mkuu wa jeshi, amepanda awazike waliouawa, akiisha kumpiga kila mwanamume wa Edomu,
16. (kwa kuwa Yoabu alikaa huko miezi sita pamoja na Israeli wote, hata alipompoteza kila mwanamume wa Edomu);
17. yule Hadadi alikimbia, yeye na Waedomi wengine, watumishi wa baba yake, pamoja naye, waende Misri; yule Hadadi akali ni mtoto mdogo.
18. Wakaondoka katika Midiani, wakafika Parani; wakachukua pamoja nao watu toka Parani, wakafika Misri, kwa Farao mfalme wa Misri; aliyempa nyumba, akamwamria vyakula, akampa mashamba.
19. Hadadi akapendeza sana machoni pa Farao, hata akamwoza umbu la mkewe, umbu la Tapenesi aliyekuwa malkia.
20. Naye huyo umbu la Tapenesi akamzalia Genubathi mwanawe, ambaye Tapenesi alimlea nyumbani mwa Farao; naye Genubathi akawako nyumbani mwa Farao pamoja na wana wa Farao.