1 Fal. 1:29-40 Swahili Union Version (SUV)

29. Naye mfalme akaapa, akasema, BWANA aishivyo, aliyenikomboa roho yangu katika shida zote,

30. hakika yake nitafanya leo kama vile nilivyokuapia kwa BWANA, Mungu wa Israeli, nikasema, Kwa yakini Sulemani mwanao atamiliki baada yangu, naye ndiye atakayeketi katika kiti changu cha enzi badala yangu.

31. Ndipo Bath-sheba akainama kifudifudi, akamsujudia mfalme, akasema, Bwana wangu mfalme Daudi na aishi milele.

32. Naye mfalme Daudi akasema, Niitie Sadoki, kuhani, na Nathani, nabii, na Benaya, mwana wa Yehoyada. Nao wakaingia ndani mbele ya mfalme.

33. Naye mfalme akawaambia, Twaeni pamoja nanyi watumishi wa bwana wenu, mkampandishe Sulemani mwanangu juu ya nyumbu wangu mimi mkamtelemshe mpaka Gihoni;

34. kisha Sadoki, kuhani, na Nathani, nabii, na wamtie mafuta huko, awe mfalme juu ya Israeli; kapigeni panda, mkaseme, Mfalme Sulemani na aishi!

35. Kisha pandeni juu nyuma yake, naye atakuja ili aketi katika kiti changu cha enzi; kwa maana atakuwa mfalme badala yangu; ndiye niliyemweka awamiliki Israeli na Yuda.

36. Basi Benaya, mwana wa Yehoyada, akamjibu mfalme, akasema, Amina; BWANA, Mungu na bwana wangu mfalme, na aseme vivyo hivyo.

37. Kama vile BWANA alivyokuwa pamoja na bwana wangu mfalme, kadhalika na awe pamoja na Sulemani, na kufanya kiti chake cha enzi kuwa kitukufu kuliko kiti cha enzi cha bwana wangu mfalme Daudi.

38. Basi wakashuka Sadoki, kuhani, na Nathani, nabii, na Benaya, mwana wa Yehoyada, na Wakerethi, na Wapelethi, wakampandisha Sulemani juu ya nyumbu wa mfalme Daudi, wakampeleka mpaka Gihoni.

39. Na Sadoki, kuhani, akatwaa ile pembe ya mafuta katika Hema, akamtia Sulemani mafuta. Nao wakapiga panda; na watu wote wakasema, Mfalme Sulemani na aishi!

40. Kisha watu wote wakapanda juu nyuma yake, watu wakapiga mazomari, wakafurahi furaha kubwa mno, hata nchi ikapasuka kwa sauti zao.

1 Fal. 1