1 Fal. 1:23-34 Swahili Union Version (SUV)

23. Wakamwambia mfalme wakasema, Tazama, Nathani, nabii. Naye alipoingia ndani mbele ya mfalme, akamsujudia kifudifudi.

24. Nathani akasema, Ee mfalme, bwana wangu, je! Wewe umesema ya kwamba, Adonia atamiliki baada yangu, ndiye atakayeketi katika kiti changu cha enzi?

25. Maana leo ameshuka, na kuchinja ng’ombe, na vinono, na kondoo tele, naye amewaita wana wote wa mfalme, na majemadari wa jeshi, na Abiathari, kuhani; na tazama, wanakula na kunywa mbele yake, wakisema, Na aishi mfalme Adonia!

26. Walakini mimi, mimi mtumishi wako, na Sadoki, kuhani, na Benaya, mwana wa Yehoyada, na Sulemani, mtumishi wako, hakutuita sisi.

27. Je! Bwana wangu mfalme ndiye aliyelitenda jambo hili, bila kutujulisha sisi watumishi wako ni nani atakayeketi katika kiti cha enzi cha bwana wangu mfalme baada yake?

28. Ndipo mfalme Daudi akajibu, akasema, Niitieni Bath-sheba. Basi akaingia ndani kwa mfalme, akasimama mbele ya mfalme.

29. Naye mfalme akaapa, akasema, BWANA aishivyo, aliyenikomboa roho yangu katika shida zote,

30. hakika yake nitafanya leo kama vile nilivyokuapia kwa BWANA, Mungu wa Israeli, nikasema, Kwa yakini Sulemani mwanao atamiliki baada yangu, naye ndiye atakayeketi katika kiti changu cha enzi badala yangu.

31. Ndipo Bath-sheba akainama kifudifudi, akamsujudia mfalme, akasema, Bwana wangu mfalme Daudi na aishi milele.

32. Naye mfalme Daudi akasema, Niitie Sadoki, kuhani, na Nathani, nabii, na Benaya, mwana wa Yehoyada. Nao wakaingia ndani mbele ya mfalme.

33. Naye mfalme akawaambia, Twaeni pamoja nanyi watumishi wa bwana wenu, mkampandishe Sulemani mwanangu juu ya nyumbu wangu mimi mkamtelemshe mpaka Gihoni;

34. kisha Sadoki, kuhani, na Nathani, nabii, na wamtie mafuta huko, awe mfalme juu ya Israeli; kapigeni panda, mkaseme, Mfalme Sulemani na aishi!

1 Fal. 1