29. Tumesikia juu ya kiburi cha Moabu;Moabu ana majivuno sana.Tumesikia juu ya kujiona, kiburi na majivuno yake;tumesikia jinsi anavyojigamba moyoni.
30. “Nami Mwenyezi-Mungu nasema:Najua ufidhuli wake;Majivuno yake ni ya bure,na matendo yake si kitu.
31. Kwa hiyo ninaomboleza juu ya Moabu,ninalia kwa ajili ya Wamoabu wote,naomboleza juu ya watu wa Kir-heresi.
32. Nakulilia wewe bustani ya Sibmakuliko hata watu wa Yazeri.Matawi yako yametandampaka ngambo ya bahari ya Chumviyakafika hata mpaka Yazeri.Lakini mwangamizi ameyakumbamatunda yako ya kiangazi na zabibu zako.
33. Furaha na shangwe zimeondolewakutoka nchi ya Moabu yenye rutuba.Nimeikomesha divai kutoka mashinikizohakuna mtu anayekamua zabibu kwa shangwe;kelele zinazosikika si za shangwe.
34. “Kilio cha watu wa Heshboni chasikika huko Eleale mpaka Yahazi; kinaenea kutoka Soari mpaka Horonaimu na hata Eglath-shelishiya. Hata maji ya kijito Nimrimu yamekauka.
35. Nami nitamfutilia mbali kila mtu katika Moabu ambaye anatambikia vilimani na kumfukizia ubani mungu wake.
36. “Kwa hiyo, moyo wangu unaomboleza juu ya watu wa Moabu na watu wa Kir-heresi, kama mpiga zumari mazishini; maana hata mali yote waliyojipatia imeangamia.
37. Kila mtu amenyoa upara na ndevu zake. Wote wamejikatakata mikononi na viunoni wamevaa mavazi ya gunia.
38. Juu ya nyumba za Moabu na katika viwanja vyao hakuna kinachosikika ila tu maombolezo. Mimi nimemvunja Moabu kama chombo kisichotakiwa na mtu. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.
39. Tazama alivyovunjika! Tazama wanavyoomboleza! Ajabu jinsi Moabu alivyorudi nyuma kwa aibu! Moabu amekuwa kichekesho na kioja kwa jirani zake wote.”
40. Mwenyezi-Mungu asema hivi:“Tazama, taifa litaruka kasi kuivamia Moabu,kama tai aliyekunjua mabawa yake.
41. Miji yake itatekwa,ngome zitachukuliwa.Siku hiyo mioyo ya wanajeshi wa Moabu,itaogopa kama mwanamke anayejifungua.
42. Wamoabu wataangamizwa, wasiwe tena taifa,kwa sababu walijikweza dhidi ya Mwenyezi-Mungu.
43. Kitisho, mashimo na mtego,vinawasubiri enyi watu wa Moabu.Nasema mimi Mwenyezi-Mungu.
44. Atakayetoroka kitishoatatumbukia shimoni;atakayetoka shimoniatanaswa mtegoni.Kwa maana nitaleta mambo hayo juu ya Moabu,katika mwaka wao wa adhabu.Nasema mimi Mwenyezi-Mungu.
45. Wakimbizi wachovu wanatua Heshboni kutaka usalama,maana moto umezuka huko mjini;mwali wa moto toka ikulu ya mfalme Sihoni;umeteketeza mipaka ya Moabu,umeunguza milima yao hao watukutu.
46. Ole wenu watu wa Moabu!Watu wa Kemoshi sasa mmeangamizwa,wana wenu wamechukuliwa mateka,binti zenu wamepelekwa uhamishoni.