9. Utakuwaje kama mtu uliyechanganyikiwa,kama shujaa asiyeweza kusaidia mtu?Lakini wewe ee Mwenyezi-Mungu, u pamoja nasi;sisi twaitwa kwa jina lako, usituache.”
10. Mwenyezi-Mungu asema hivi juu ya watu hawa:“Kweli wamependa sana kutangatanga,wala hawakujizuia;kwa hiyo mimi Mwenyezi-Mungu siwapokei.Sasa nitayakumbuka makosa yao,na kuwaadhibu kwa dhambi zao.”
11. Mwenyezi-Mungu aliniambia hivi: “Usiwaombee watu hawa fanaka.
12. Hata wakifunga, sitayasikiliza maombi yao, na hata wakinitolea sadaka za kuteketeza na za nafaka, mimi sitazikubali. Bali nitawaangamiza kwa upanga, njaa na tauni.”
13. Kisha mimi nikasema, “Tazama, ee Bwana Mwenyezi-Mungu! Manabii wanawaambia watu hawa kwamba hapatakuwa na vita wala njaa, kwa sababu umeahidi kuwa patakuwa na amani tu katika nchi yetu.”