24. Gideoni akamjengea Mwenyezi-Mungu madhabahu huko na kuyaita, “Mwenyezi-Mungu ni Amani.” Madhabahu hiyo iko huko Ofra, mji wa Wabiezeri, mpaka leo.
25. Usiku huo, Mwenyezi-Mungu akamwambia Gideoni, “Chukua fahali mmoja wa baba yako, fahali yule wa pili wa umri wa miaka saba. Bomoa madhabahu ya Baali aliyo nayo baba yako na kuvunja sanamu ya Ashera iliyo karibu nayo.
26. Halafu, unijengee mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, madhabahu nzuri juu ya mwinuko huu. Kisha unitolee sadaka ya kuteketezwa ya yule fahali wa pili ukitumia kuni za ile sanamu ya Ashera uliyoivunja.”
27. Basi, Gideoni akachukua watumishi wake kumi, akafanya kama alivyoagizwa na Mwenyezi-Mungu. Lakini kwa kuwa aliiogopa jamaa yake na watu wa mjini, badala ya kufanya hayo mchana, alifanya wakati wa usiku.
28. Wakazi wa mji walipoamka asubuhi na mapema waliona madhabahu ya Baali na sanamu ya Ashera iliyokuwa karibu nayo vimeharibiwa. Yule fahali wa pili alikuwa ameteketezwa juu ya madhabahu iliyokuwa imejengwa mahali hapo.
29. Wakaulizana, “Nani amefanya jambo hili?” Walipofanya uchunguzi wakagundua kwamba Gideoni mwana wa Yoashi ndiye aliyekuwa amefanya hayo.
30. Wakazi wa mji wakamjia Yoashi, wakamwambia, “Mtoe mwanao tumuue, maana ameharibu madhabahu ya Baali na kuivunja sanamu ya Ashera iliyokuwa karibu nayo.”
31. Yoashi akawaambia wale wote waliomkabili, “Je, mnamtetea Baali? Je, mtamwokoa? Yeyote atakayemtetea atauawa kabla ya mapambazuko. Kama Baali ni mungu, basi, na ajitetee mwenyewe maana madhabahu yake imebomolewa.”
32. Siku hiyo wakamwita Gideoni “Yerubaali” maana yake, “Baali na ajitetee mbele yake”, maana aliibomoa madhabahu ya Baali.
33. Wamidiani, Waamaleki na watu wote wanaokaa kando ya mto Yordani wakapiga kambi zao katika bonde la Yezreeli.
34. Lakini roho ya Mwenyezi-Mungu ikamjia Gideoni. Gideoni akapiga tarumbeta kuwaita Wabiezeri waje kumfuata.