Waamuzi 6:12-30 Biblia Habari Njema (BHN)

12. Malaika wa Mwenyezi-Mungu akamtokea, akamwambia, “Mwenyezi-Mungu yuko pamoja nawe, ewe shujaa.”

13. Gideoni akamwambia, “Ee Bwana wangu, ikiwa Mwenyezi-Mungu yuko pamoja nasi, mbona mambo haya yote yametupata? Yako wapi matendo yake ya ajabu ambayo wazee wetu walitusimulia, wakisema: ‘Mwenyezi-Mungu ndiye aliyetutoa nchini Misri.’ Lakini sasa Mwenyezi-Mungu ametutupa na kututia mikononi mwa Wamidiani!”

14. Mwenyezi-Mungu akamgeukia, akamwambia, “Nenda kwa uwezo ulio nao, ukaikomboe Israeli kutoka Wamidiani. Ni mimi ninayekutuma.”

15. Gideoni akamjibu, “Tafadhali Bwana, nitawezaje kuikomboa Israeli? Ukoo wangu ndio dhaifu zaidi katika kabila la Manase, na mimi mwenyewe ni mdogo kabisa katika jamaa yetu!”

16. Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Nitakuwa pamoja nawe; nawe utawaangamiza Wamidiani kana kwamba wangekuwa mtu mmoja.”

17. Gideoni akamwambia, “Basi, ikiwa nimepata fadhili kwako, nioneshe ishara ili nijue kuwa ni wewe kweli uliyezungumza nami.

18. Nakuomba usiondoke hapa mpaka nitakaporudi na kukuletea zawadi yangu na kuiweka mbele yako.”Naye akamjibu, “Nitakaa hapa mpaka utakaporudi.”

19. Gideoni akaenda nyumbani mwake, akatayarisha mwanambuzi na mikate isiyotiwa chachu kutoka debe la unga; akatia nyama ndani ya kikapu na mchuzi ndani ya chungu, kisha akampelekea chini ya mwaloni, akampa.

20. Malaika wa Mungu akamwambia, “Chukua nyama na mikate isiyotiwa chachu uviweke juu ya mwamba huu. Halafu tia mchuzi juu ya mikate na nyama.” Naye akafanya hivyo.

21. Malaika wa Mwenyezi-Mungu akanyosha fimbo yake, akagusa nyama na mikate kwa ncha ya fimbo. Ghafla, moto ukatoka mwambani, ukateketeza nyama na mikate. Mara malaika wa Mwenyezi-Mungu akatoweka mbele yake.

22. Ndipo Gideoni akatambua kwamba huyo alikuwa malaika wa Mwenyezi-Mungu; akasema, “Ole wangu, ee Bwana Mwenyezi-Mungu, maana nimemwona malaika wako uso kwa uso.”

23. Lakini Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Amani iwe nawe! Usiogope, hutakufa.”

24. Gideoni akamjengea Mwenyezi-Mungu madhabahu huko na kuyaita, “Mwenyezi-Mungu ni Amani.” Madhabahu hiyo iko huko Ofra, mji wa Wabiezeri, mpaka leo.

25. Usiku huo, Mwenyezi-Mungu akamwambia Gideoni, “Chukua fahali mmoja wa baba yako, fahali yule wa pili wa umri wa miaka saba. Bomoa madhabahu ya Baali aliyo nayo baba yako na kuvunja sanamu ya Ashera iliyo karibu nayo.

26. Halafu, unijengee mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, madhabahu nzuri juu ya mwinuko huu. Kisha unitolee sadaka ya kuteketezwa ya yule fahali wa pili ukitumia kuni za ile sanamu ya Ashera uliyoivunja.”

27. Basi, Gideoni akachukua watumishi wake kumi, akafanya kama alivyoagizwa na Mwenyezi-Mungu. Lakini kwa kuwa aliiogopa jamaa yake na watu wa mjini, badala ya kufanya hayo mchana, alifanya wakati wa usiku.

28. Wakazi wa mji walipoamka asubuhi na mapema waliona madhabahu ya Baali na sanamu ya Ashera iliyokuwa karibu nayo vimeharibiwa. Yule fahali wa pili alikuwa ameteketezwa juu ya madhabahu iliyokuwa imejengwa mahali hapo.

29. Wakaulizana, “Nani amefanya jambo hili?” Walipofanya uchunguzi wakagundua kwamba Gideoni mwana wa Yoashi ndiye aliyekuwa amefanya hayo.

30. Wakazi wa mji wakamjia Yoashi, wakamwambia, “Mtoe mwanao tumuue, maana ameharibu madhabahu ya Baali na kuivunja sanamu ya Ashera iliyokuwa karibu nayo.”

Waamuzi 6