Ezekieli 41:7-14 Biblia Habari Njema (BHN)

7. Kwa upande, zile kuta za hekalu zikitazamwa kutokea nje, zilionekana kuwa na unene uleule toka chini hadi juu. Mkabala na ukuta wa nje wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu, nje ya vyumba, kulikuwa na ngazi mbili, ambazo zilifanya iwe rahisi kwenda juu kutokea ghorofa ya chini hadi ile ya juu.

8. Kisha, nikaona kuwa hekalu lilikuwa na sakafu iliyonyanyuliwa kulizunguka, nayo ilikuwa ndio msingi wa zile ghorofa tatu mkabala na hekalu, kimo cha msingi wa ghorofa hizo ulikuwa sawa na ule ufito wa kupimia, mita tatu.

9. Unene wa ukuta wa nje wa vyumba vya ndani ulikuwa mita mbili u nusu. Nafasi wazi kati ya vyumba vya pembeni mkabala na hekalu

10. na vyumba vya walinzi vilikuwa na upana wa mita 10, kuzunguka hekalu.

11. Kulikuwa na milango kwenye vyumba vya pembeni kutokea kwenye uwanja, mmoja upande wa kaskazini na mwingine upande wa kusini. Na msingi uliounganishwa na uwanja ulikuwa na upana wa mita 2.5.

12. Mwishoni kabisa mwa uwanja, upande wa magharibi kulikuwa na jengo lenye urefu wa mita 45 na upana wa mita 35. Kuta zake zilikuwa na unene wa mita 2.5.

13. Yule mtu akapima upande wa nje wa hekalu nao ulikuwa na urefu wa mita 50. Tokea nyuma ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu kupitia ile nafasi ya kupitia, hadi mwisho wake, upande wa magharibi, umbali wake ulikuwa pia mita 50.

14. Urefu mbele ya hekalu tangu upande huu hadi upande huu ukichanganya na ile nafasi wazi, ulikuwa pia mita 50.

Ezekieli 41