1. Neno la BWANA wa majeshi likanijia, kusema,
2. BWANA wa majeshi asema hivi, Mimi nina wivu kwa ajili ya Sayuni, wivu mkuu, nami nina wivu kwa ajili yake kwa ghadhabu kuu.
3. BWANA asema hivi, Mimi nimerudi Sayuni, nami nitakaa katikati ya Yerusalemu; na Yerusalemu utaitwa, Mji wa kweli; na Mlima wa BWANA wa majeshi utaitwa, Mlima mtakatifu.
4. BWANA wa majeshi asema hivi, Wazee wanaume na wazee wanawake watakaa tena katika njia za Yerusalemu, kila mtu ana mkongojo wake mkononi, kwa kuwa ni mzee sana.
5. Na hizo njia za mji zitajaa wavulana, na wasichana, wakicheza katika njia zake.