Zek. 8:1-13 Swahili Union Version (SUV)

1. Neno la BWANA wa majeshi likanijia, kusema,

2. BWANA wa majeshi asema hivi, Mimi nina wivu kwa ajili ya Sayuni, wivu mkuu, nami nina wivu kwa ajili yake kwa ghadhabu kuu.

3. BWANA asema hivi, Mimi nimerudi Sayuni, nami nitakaa katikati ya Yerusalemu; na Yerusalemu utaitwa, Mji wa kweli; na Mlima wa BWANA wa majeshi utaitwa, Mlima mtakatifu.

4. BWANA wa majeshi asema hivi, Wazee wanaume na wazee wanawake watakaa tena katika njia za Yerusalemu, kila mtu ana mkongojo wake mkononi, kwa kuwa ni mzee sana.

5. Na hizo njia za mji zitajaa wavulana, na wasichana, wakicheza katika njia zake.

6. BWANA wa majeshi asema hivi, Ingawa hili ni neno lililo gumu mbele ya macho ya mabaki ya watu hawa katika siku hizo, je! Liwe neno gumu mbele ya macho yangu? Asema BWANA wa majeshi.

7. BWANA wa majeshi asema hivi, Tazama, nitawaokoa watu wangu toka nchi ya mashariki, na toka nchi ya magharibi;

8. nami nitawaleta, nao watakaa katikati ya Yerusalemu; nao watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao, katika kweli na katika haki.

9. BWANA wa majeshi asema hivi, Mikono yenu na iwe hodari, ninyi mnaosikia siku hizi maneno haya kwa vinywa vya manabii, waliokuwapo siku hiyo ulipowekwa msingi wa nyumba ya BWANA wa majeshi; yaani, hekalu hilo; ili lijengwe.

10. Maana kabla ya siku zile hapakuwa na ijara kwa mwanadamu, wala hapakuwa na ijara kwa mnyama; wala hapakuwa na amani kwake yeye aliyetoka, wala kwake yeye aliyeingia, kwa sababu ya adui; nami nalimwacha kila mtu kugombana na jirani yake.

11. Lakini sasa sitakuwa kwa mabaki ya watu hawa kama nilivyokuwa siku zile za kwanza, asema BWANA wa majeshi.

12. Kwa maana itakuwako mbegu ya amani; mzabibu utatoa matunda yake, nayo ardhi itatoa mazao yake, na hizo mbingu zitatoa umande wake; nami nitawarithisha mabaki ya watu hawa vitu hivi vyote.

13. Kisha itakuwa, kama vile mlivyokuwa laana katika mataifa, Ee nyumba ya Yuda, na nyumba ya Israeli, ndivyo nitakavyowaokoa, nanyi mtakuwa baraka; msiogope, lakini mikono yenu na iwe hodari.

Zek. 8