Zab. 78:55-67 Swahili Union Version (SUV)

55. Akawafukuza mataifa mbele yao,Akawapimia urithi kwa kamba,Na kuwakalisha kabila za Israeli katika hema zao.

56. Lakini walimjaribu Mungu Aliye juu, wakamwasi,Wala hawakuzishika shuhuda zake.

57. Bali walirudi nyuma, wakahaini kama baba zao;Wakaepea kama upinde usiofaa.

58. Wakamkasirisha kwa mahali pao pa juu,Wakamtia wivu kwa sanamu zao.

59. Mungu akasikia, akaghadhibika,Akamkataa Israeli kabisa.

60. Akaiacha maskani ya Shilo,Hema aliyoiweka katikati ya wanadamu;

61. Akaziacha nguvu zake kutekwa,Na fahari yake mkononi mwa mtesi.

62. Akawatoa watu wake wapigwe kwa upanga;Akaughadhibikia urithi wake.

63. Moto ukawala vijana wao,Wanawali wao hawakuimbiwa nyimbo za arusi,

64. Makuhani wao walianguka kwa upanga,Wala wajane wao hawakuomboleza.

65. Ndipo Bwana alipoamka kama aliyelala usingizi,Kama shujaa apigaye kelele sababu ya mvinyo;

66. Akawapiga watesi wake akawarudisha nyuma,Akawatia aibu ya milele.

67. Ila akaikataa hema ya Yusufu;Wala hakuichagua kabila ya Efraimu.

Zab. 78