51. Akampiga kila mzaliwa wa kwanza wa Misri,Malimbuko ya nguvu katika hema za Hamu.
52. Bali aliwaongoza watu wake kama kondoo,Akawachunga kama kundi jangwani.
53. Hao akawachukua salama wala hawakuogopa,Bali bahari iliwafunikiza adui zao.
54. Akawapeleka hadi mpaka wake mtakatifu,Mlima alioununua kwa mkono wake wa kuume.
55. Akawafukuza mataifa mbele yao,Akawapimia urithi kwa kamba,Na kuwakalisha kabila za Israeli katika hema zao.
56. Lakini walimjaribu Mungu Aliye juu, wakamwasi,Wala hawakuzishika shuhuda zake.
57. Bali walirudi nyuma, wakahaini kama baba zao;Wakaepea kama upinde usiofaa.
58. Wakamkasirisha kwa mahali pao pa juu,Wakamtia wivu kwa sanamu zao.
59. Mungu akasikia, akaghadhibika,Akamkataa Israeli kabisa.
60. Akaiacha maskani ya Shilo,Hema aliyoiweka katikati ya wanadamu;
61. Akaziacha nguvu zake kutekwa,Na fahari yake mkononi mwa mtesi.
62. Akawatoa watu wake wapigwe kwa upanga;Akaughadhibikia urithi wake.
63. Moto ukawala vijana wao,Wanawali wao hawakuimbiwa nyimbo za arusi,
64. Makuhani wao walianguka kwa upanga,Wala wajane wao hawakuomboleza.
65. Ndipo Bwana alipoamka kama aliyelala usingizi,Kama shujaa apigaye kelele sababu ya mvinyo;