Zab. 18:27-42 Swahili Union Version (SUV)

27. Maana Wewe utawaokoa watu wanaoonewa,Na macho ya kiburi utayadhili.

28. Kwa kuwa Wewe unaiwasha taa yangu;BWANA Mungu wangu aniangazia giza langu.

29. Maana kwa msaada wako nafuatia jeshi,Kwa msaada wa Mungu wangu naruka ukuta.

30. Mungu, njia yake ni kamilifu,Ahadi ya BWANA imehakikishwa,Yeye ndiye ngao yao.Wote wanaomkimbilia.

31. Maana ni nani aliye Mungu ila BWANA?Ni nani aliye mwamba ila Mungu wetu?

32. Mungu ndiye anifungaye mshipi wa nguvu,Naye anaifanya kamilifu njia yangu.

33. Miguu yangu anaifanya kuwa ya kulungu,Na kunisimamisha mahali pangu pa juu.

34. Ananifundisha mikono yangu vita,Mikono yangu ikaupinda upinde wa shaba.

35. Nawe umenipa ngao ya wokovu wako,Mkono wako wa kuume umenitegemeza,Na unyenyekevu wako umenikuza.

36. Umezifanyizia nafasi hatua zangu,Na miguu yangu haikuteleza.

37. Nitawafuatia adui zangu na kuwapata,Wala sitarudi nyuma hata wakomeshwe.

38. Nitawapiga-piga wasiweze kusimama,Wataanguka chini ya miguu yangu.

39. Nawe hunifunga mshipi wa nguvu kwa vita,Hunitiishia chini yangu walioniondokea.

40. Naam, adui zangu umewafanya wanipe visogo,Nao walionichukia nimewakatilia mbali.

41. Walipiga yowe, lakini hakuna wa kuokoa,Walimwita BWANA lakini hakuwajibu,

42. Nikawaponda kama mavumbi mbele ya upepo,Nikawatupa nje kama matope ya njiani.

Zab. 18