5. Kisha itakuwa watakapopiga hizo pembe za kondoo waume kwa nguvu, nanyi mtakaposikia sauti ya tarumbeta, watu wote watapiga kelele kwa sauti kuu; na ukuta wa mji utaanguka chini pale pale, na hao watu watapanda, kila mtu akiendelea mbele kukabili.
6. Bali Yoshua, mwana wa Nuni, akawaita makuhani, akawaambia, Lichukueni sanduku la agano, tena makuhani saba na wachukue tarumbeta saba za pembe za kondoo waume mbele ya sanduku la BWANA.
7. Naye akawaambia watu, Piteni mbele, mkauzunguke mji, na hao watu wenye silaha na watangulie mbele ya sanduku la BWANA.
8. Basi ikawa Yoshua alipokwisha kusema na watu, wale makuhani saba, wenye kuzichukua tarumbeta saba za pembe za kondoo waume mbele za BWANA, wakatangulia, wakazipiga hizo tarumbeta; nalo sanduku la agano la BWANA likawafuata.
9. Wale watu wenye silaha walikwenda mbele ya hao makuhani waliozipiga tarumbeta, na wale waliokuwa nyuma wakalifuata hilo sanduku; makuhani wakizipiga tarumbeta walipokuwa wakienda.
10. Yoshua akawaamuru watu, akasema Msipige kelele, wala sauti zenu zisisikiwe, wala neno lo lote lisitoke kinywani mwenu, hata siku ile nitakapowaamuru kupiga kelele, ndipo mtakapopiga kelele.
11. Basi akalipeleka sanduku la BWANA liuzunguke huo mji, likauzunguka mara moja, kisha wakaenda kambini wakakaa kambini.
12. Yoshua akaondoka asubuhi na mapema, nao makuhani wakalichukua sanduku la BWANA.
13. Na wale makuhani saba wakazichukua tarumbeta saba za pembe za kondoo waume mbele ya sanduku la BWANA, wakaendelea wakazipiga tarumbeta; nao watu wenye silaha wakawatangulia, na hao waliokuwa nyuma wakalifuata sanduku la BWANA; makuhani wakizipiga tarumbeta walipokuwa wakienda.