Yoe. 2:15-22 Swahili Union Version (SUV)

15. Pigeni tarumbeta katika Sayuni,Takaseni saumu, kusanyeni kusanyiko kuu;

16. Kusanyeni watu, litakaseni kusanyiko,Kusanyeni wazee, kusanyeni watoto,Na hao wanyonyao maziwa;Bwana arusi na atoke chumbani mwake,Na bibi arusi katika hema yake.

17. Hao makuhani, wahudumu wa BWANA, na walieKati ya patakatifu na madhabahu,Na waseme, Uwaachilie watu wako, Ee BWANA,Wala usiutoe urithi wako upate aibu,Hata mataifa watawale juu yao;Kwani waseme kati ya watu, Yuko wapi Mungu wao?

18. Hapo ndipo BWANA alipoona wivu kwa ajili ya nchi yake, akawahurumia watu wake.

19. BWANA akajibu, akawaambia watu wake; Tazameni, nitawaletea nafaka, na divai, na mafuta, nanyi mtashiba kwa vitu hivyo; wala sitawafanya tena kuwa aibu kati ya mataifa;

20. lakini jeshi lililotoka kaskazini nitaliondolea mbali nanyi, nami nitalifukuza mpaka nchi ya ukame na ukiwa; sehemu yake iliyo mbele itaingia katika bahari ya mashariki, na sehemu yake iliyo nyuma itaingia katika bahari ya magharibi; na uvundo wake utapanda juu, na harufu yake mbaya itapanda juu, kwa sababu ametenda mambo makubwa.

21. Ee nchi, usiogope; furahi na kushangilia; kwa kuwa BWANA ametenda mambo makuu.

22. Msiogope, enyi wanyama wa kondeni; maana malisho ya jangwani yanatoa miche, na huo mti unazaa matunda yake, mtini na mzabibu inatoa nguvu zake.

Yoe. 2