24. Amin, amin, nawaambia, Chembe ya ngano isipoanguka katika nchi, ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali ikifa, hutoa mazao mengi.
25. Yeye aipendaye nafsi yake ataiangamiza; naye aichukiaye nafsi yake katika ulimwengu huu ataisalimisha hata uzima wa milele.
26. Mtu akinitumikia, na anifuate; nami nilipo, ndipo na mtumishi wangu atakapokuwapo. Tena mtu akinitumikia, Baba atamheshimu.
27. Sasa roho yangu imefadhaika; nami nisemeje? Baba, uniokoe katika saa hii? Lakini ni kwa ajili ya hayo nilivyoifikia saa hii.
28. Baba, ulitukuze jina lako. Basi ikaja sauti kutoka mbinguni, Nimelitukuza, nami nitalitukuza tena.
29. Basi mkutano uliosimama karibu wakasikia, walisema ya kwamba kumekuwa ngurumo; wengine walisema, Malaika amesema naye.
30. Yesu akajibu, akasema, Sauti hiyo haikuwako kwa ajili yangu, bali kwa ajili yenu.
31. Sasa hukumu ya ulimwengu huu ipo; sasa mkuu wa ulimwengu huu atatupwa nje.
32. Nami nikiinuliwa juu ya nchi, nitawavuta wote kwangu.
33. Aliyanena hayo akionyesha ni mauti gani atakayokufa.
34. Basi mkutano wakamjibu, Sisi tumesikia katika torati ya kwamba Kristo adumu hata milele; nawe wasemaje ya kwamba imempasa Mwana wa Adamu kuinuliwa? Huyu Mwana wa Adamu ni nani?
35. Basi Yesu akawaambia, Nuru ingaliko pamoja nanyi muda kidogo. Enendeni maadamu mnayo nuru hiyo, giza lisije likawaweza; maana aendaye gizani hajui aendako.
36. Maadamu mnayo nuru, iaminini nuru hiyo, ili mpate kuwa wana wa nuru.Hayo aliyasema Yesu, akaenda zake, akajificha wasimwone.
37. Walakini ajapokuwa amefanya ishara nyingi namna hiyo mbele yao, hawakumwamini;
38. ili litimie lile neno la nabii Isaya alilolisema,Bwana, ni nani aliyezisadiki habari zetu;Na mkono wa Bwana amefunuliwa nani?
39. Ndiyo sababu wao hawakuweza kusadiki; kwa maana Isaya alisema tena,
40. Amewapofusha macho,Ameifanya mizito mioyo yao;Wasije wakaona kwa macho yao,Wakafahamu kwa mioyo yao,Wakaongoka, nikawaponya.
41. Maneno hayo aliyasema Isaya, kwa kuwa aliuona utukufu wake, akataja habari zake.
42. Walakini hata katika wakuu walikuwamo wengi waliomwamini; lakini kwa sababu ya Mafarisayo hawakumkiri, wasije wakatengwa na sinagogi.
43. Kwa maana walipenda utukufu wa wanadamu kuliko utukufu wa Mungu.