4. Tena utawaambia, BWANA asema hivi, Je! Watu wataanguka, wasisimame tena? Je! Mtu atageuka aende zake, asirudi tena?
5. Mbona, basi, watu hawa wa Yerusalemu wamegeuka waende nyuma, wasikome kugeuka hivyo? Hushika udanganyifu sana, hukataa kurudi.
6. Nalisikiliza nikasikia, lakini walisema yasiyo sawa; hapana mtu aliyetubia maovu yake, akisema, Nimefanya nini? Kila mtu hurudia mwendo wake mwenyewe, kama farasi aendavyo kasi vitani.
7. Naam, koikoi angani ajua nyakati zake zilizoamriwa; na hua na mbayuwayu na korongo huangalia wakati wa kuja kwao; bali watu wangu hawazijui amri za BWANA.
8. Mwasemaje, Sisi tuna akili, na torati ya BWANA tunayo pamoja nasi? Lakini, tazama, kalamu yenye uongo ya waandishi imeifanya kuwa uongo.
9. Wenye hekima wametahayari, wamefadhaika na kushikwa; tazama, wamelikataa neno la BWANA, wana akili gani ndani yao?
10. Basi, kwa hiyo nitawapa watu wengine wake zao na mashamba yao nitawapa wale watakaowamiliki; maana kila mmoja wao, tangu aliye mdogo hata aliye mkubwa, ni mtamanifu; tangu nabii hata kuhani, kila mmoja hutenda mambo ya udanganyifu.
11. Kwa maana wameiponya jeraha ya binti ya watu wangu kwa juu-juu tu, wakisema, Amani, Amani, wala hapana amani.