18. Watoto huokota kuni, na baba zao huwasha moto, na wanawake hukanda unga, ili kumfanyizia mikate malkia wa mbinguni, na kuwamiminia miungu mingine sadaka za kinywaji, wapate kunikasirisha mimi.
19. Je! Watu hawa wanikasirisha mimi? Asema BWANA; hawajikasirishi nafsi zao, na kuzitia haya nyuso zao wenyewe?
20. Kwa hiyo, Bwana MUNGU asema hivi, Tazama, hasira yangu na ghadhabu yangu zitamwagwa juu ya mahali hapa, juu ya wanadamu, na juu ya wanyama, na juu ya miti ya mashamba, na juu ya mazao ya nchi; nayo itateketea, isizimike.
21. BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Tieni sadaka zenu za kuteketezwa pamoja na dhabihu zenu, mkale nyama.
22. Maana sikusema na baba zenu, wala sikuwaamuru kwa habari za sadaka za kuteketezwa na dhabihu, siku ile nilipowatoa katika nchi ya Misri;
23. lakini naliwaamuru neno hili, nikisema, Sikilizeni sauti yangu, nami nitakuwa Mungu wenu nanyi mtakuwa watu wangu; mkaende katika njia ile yote nitakayowaamuru mpate kufanikiwa.
24. Lakini hawakusikiliza, wala kutega sikio lao, bali walikwenda kwa mashauri yao wenyewe, na kwa ushupavu wa mioyo yao mibaya, wakaenda nyuma wala si mbele.
25. Tokea siku ile baba zenu walipotoka katika nchi ya Misri hata leo, nimewatuma watumishi wangu wote manabii kwenu ninyi, nikiamka mapema kila siku, na kuwatuma.
26. Lakini hawakunisikiliza, wala kutega sikio lao; bali walifanya shingo yao kuwa ngumu; walitenda mabaya kuliko baba zao.
27. Nawe utawaambia maneno hayo yote; lakini hawatakusikiliza, nawe utawaita; lakini hawatakuitikia.
28. Nawe utawaambia, Taifa hili ndilo lisilosikiliza sauti ya BWANA, Mungu wao, wala kupokea mafundisho; uaminifu umepotea, umekatiliwa mbali na vinywa vyao.
29. Zikate nywele zako, Ee Yerusalemu, uzitupe,Ukafanye maombolezo juu ya vilele vya milima;Kwa maana BWANA amekikataa na kukitupaKizazi cha ghadhabu yake.
30. Maana wana wa Yuda wametenda yaliyo maovu machoni pangu, asema BWANA; wameweka machukizo yao ndani ya nyumba hiyo, iitwayo kwa jina langu, hata kuitia unajisi.