Yer. 6:4-10 Swahili Union Version (SUV)

4. Takaseni vita juu yake; inukeni, na tupande juu wakati wa adhuhuri. Ole wetu, kwa kuwa mchana umeanza kupungua, vivuli vya jioni vinazidi kuwa virefu.

5. Inukeni, na tupande juu wakati wa usiku, tukayaharibu majumba yake.

6. Maana BWANA wa majeshi asema hivi, Jikatieni miti, mfanyize boma juu ya Yerusalemu. Mji huu ni mji unaojiliwa; dhuluma tupu imo ndani yake.

7. Kama vile kisima kitoavyo maji yake, ndivyo utoavyo uovu wake; jeuri na kuharibu kwasikiwa ndani yake; ugonjwa na jeraha zi mbele zangu daima.

8. Uadhibishwe, Ee Yerusalemu, nafsi yangu, isije ikafarakana nawe; nisije nikakufanya ukiwa, nchi isiyokaliwa na watu.

9. BWANA wa majeshi asema hivi, Wataokota mabaki ya Israeli kama mzabibu; rudisha mkono wako ndani ya vikapu, kama mchuma zabibu.

10. Niseme na nani na kushuhudia, wapate kusikia? Tazama, sikio lao halikutahiriwa, wala hawawezi kusikiliza; tazama, neno la BWANA limekuwa matukano kwao; hawalifurahii.

Yer. 6