1. Kimbieni mpate kuwa salama, enyi wana wa Benyamini; tokeni katika Yerusalemu, pigeni tarumbeta katika Tekoa, simamisheni ishara juu ya Beth-hakeremu; kwa maana mabaya yanachungulia toka kaskazini, na uharibifu mkuu.
2. Binti Sayuni aliye mzuri, mwororo, nitamkatilia mbali.
3. Wachungaji na makundi yao ya kondoo watamjilia; watapiga hema zao karibu naye pande zote; watalisha kila mmoja mahali pake.
4. Takaseni vita juu yake; inukeni, na tupande juu wakati wa adhuhuri. Ole wetu, kwa kuwa mchana umeanza kupungua, vivuli vya jioni vinazidi kuwa virefu.
5. Inukeni, na tupande juu wakati wa usiku, tukayaharibu majumba yake.
6. Maana BWANA wa majeshi asema hivi, Jikatieni miti, mfanyize boma juu ya Yerusalemu. Mji huu ni mji unaojiliwa; dhuluma tupu imo ndani yake.
7. Kama vile kisima kitoavyo maji yake, ndivyo utoavyo uovu wake; jeuri na kuharibu kwasikiwa ndani yake; ugonjwa na jeraha zi mbele zangu daima.
8. Uadhibishwe, Ee Yerusalemu, nafsi yangu, isije ikafarakana nawe; nisije nikakufanya ukiwa, nchi isiyokaliwa na watu.
9. BWANA wa majeshi asema hivi, Wataokota mabaki ya Israeli kama mzabibu; rudisha mkono wako ndani ya vikapu, kama mchuma zabibu.
10. Niseme na nani na kushuhudia, wapate kusikia? Tazama, sikio lao halikutahiriwa, wala hawawezi kusikiliza; tazama, neno la BWANA limekuwa matukano kwao; hawalifurahii.
11. Lakini nimejaa ghadhabu ya BWANA; nimechoka kwa kujizuia; imwageni juu ya watoto walio njiani, na juu ya kusanyiko la vijana pia; maana hata mume atatwaliwa pamoja na mkewe, mzee pamoja na yeye aliyetimiza siku zake.
12. Na nyumba zao zitakuwa mali za watu wengine, mashamba yao na wake zao pamoja; kwa kuwa nitaunyosha mkono wangu juu ya wenyeji wa nchi hii, asema BWANA.