17. Na nguzo za shaba zilizokuwa katika nyumba ya BWANA, na matako ya bahari ya shaba iliyokuwa katika nyumba ya BWANA, Wakaldayo walivivunja vipande vipande, wakaichukua shaba yake yote mpaka Babeli.
18. Nayo masufuria, na majembe, na makasi, na mabakuli, na miiko, na vyombo vyote vya shaba walivyokuwa wakivitumia, wakavichukua vyote.
19. Navyo vikombe, na vyombo vya kutolea majivu, na mabakuli, na masufuria, na vinara, na miiko, na vyetezo, vilivyokuwa vya dhahabu katika dhahabu, na vilivyokuwa vya fedha katika fedha, amiri wa askari walinzi akavichukua.
20. Nguzo mbili, bahari moja, na ng’ombe kumi na mbili za shaba zilizokuwa chini ya matako yake, ambavyo mfalme Sulemani aliifanyia nyumba ya BWANA; shaba ya vitu hivyo vyote ilikuwa haiwezi kupimwa kwa kuwa nyingi sana.
21. Na nguzo hizo, urefu wa nguzo moja ulikuwa dhiraa kumi na nane, na uzi wa dhiraa kumi na mbili ungeweza kuizunguka; na unene wake ulikuwa nyanda nne; nayo ilikuwa ya uvungu.
22. Nayo ilikuwa na kichwa cha shaba juu yake; na urefu wa kichwa kimoja ulikuwa dhiraa tano; palikuwa na mapambo ya wavu na makomamanga juu ya kichwa hicho pande zote; vyote vilikuwa vya shaba; nayo nguzo ya pili ilikuwa na mapambo kama hayo, na makomamanga.
23. Palikuwa na makomamanga tisini na sita katika pande zake; makomamanga; yote yalikuwa mia juu ya wavu huo pande zote.