Yer. 52:12-19 Swahili Union Version (SUV)

12. Basi katika mwezi wa tano, siku ya kumi ya mwezi, ndio mwaka wa kumi na kenda wa mfalme Nebukadreza, mfalme wa Babeli; Nebuzaradani, amiri wa askari walinzi, aliyesimama mbele ya mfalme wa Babeli, aliingia Yerusalemu.

13. Akaiteketeza nyumba ya BWANA, na nyumba ya mfalme; na nyumba zote za Yerusalemu, naam, kila nyumba kubwa aliiteketeza kwa moto.

14. Na jeshi lote la Wakaldayo, waliokuwa pamoja na huyo amiri wa askari walinzi, wakazibomoa kuta zote za Yerusalemu pande zote.

15. Kisha Nebuzaradani, amiri wa askari walinzi, akawachukua wafungwa baadhi ya watu waliokuwa maskini, na mabaki ya watu walioachwa katika mji, nao wale walioasi na kumkimbilia mfalme wa Babeli, nao mabaki ya vibarua.

16. Lakini Nebuzaradani, amiri wa askari walinzi, akawaacha watu walio maskini kabisa ili wawe watunza mizabibu na wakulima.

17. Na nguzo za shaba zilizokuwa katika nyumba ya BWANA, na matako ya bahari ya shaba iliyokuwa katika nyumba ya BWANA, Wakaldayo walivivunja vipande vipande, wakaichukua shaba yake yote mpaka Babeli.

18. Nayo masufuria, na majembe, na makasi, na mabakuli, na miiko, na vyombo vyote vya shaba walivyokuwa wakivitumia, wakavichukua vyote.

19. Navyo vikombe, na vyombo vya kutolea majivu, na mabakuli, na masufuria, na vinara, na miiko, na vyetezo, vilivyokuwa vya dhahabu katika dhahabu, na vilivyokuwa vya fedha katika fedha, amiri wa askari walinzi akavichukua.

Yer. 52