8. Babeli umeanguka na kuangamia ghafula; mpigieni yowe; twaeni zeri kwa maumivu yake; ili labda apate kuponywa.
9. Tungependa kuuponya Babeli,Lakini haukuponyeka;Mwacheni, nasi twendeni zetu,Kila mtu hata nchi yake mwenyewe;Maana hukumu yake inafika hata mbinguni,Nayo imeinuliwa kufikilia mawinguni.
10. BWANA ameitokeza haki yetu;Njoni, tutangaze katika SayuniHabari za kazi ya BWANA, Mungu wetu.
11. Inoeni hiyo mishale; zishikeni ngao kwa nguvu; BWANA ameziamsha roho za wafalme wa Wamedi; kwa sababu shauri lake ni juu ya Babeli auangamize; maana ni kisasi cha BWANA, kisasi cha hekalu lake.
12. Twekeni bendera juu ya kuta za Babeli, yatieni malindo nguvu, wawekeni walinzi, tengenezeni waviziao; kwa maana BWANA ameazimia na kutenda yote aliyoyasema juu yao wakaao Babeli.
13. Ewe ukaaye juu ya maji mengi, uliye na hazina nyingi, mwisho wako umewadia, kadiri ya tamaa zako.
14. BWANA wa majeshi ameapa kwa nafsi yake, akisema, Hakika nitakujaza watu, kama nzige, nao watapiga kelele juu yako.
15. Ameiumba dunia kwa uweza wake,Ameuthibitisha ulimwengu kwa hekima yake,Na kwa ufahamu wake amezitandika mbingu.
16. Atoapo sauti yake pana mshindo wa maji mbinguni,Naye hupandisha mawingu toka ncha za nchi;Huifanyia mvua umeme,Huutoa upepo katika hazina zake.