18. Ni ubatili tu, ni kazi za udanganyifu;Wakati wa kujiliwa kwao watapotea.
19. Yeye, Fungu la Yakobo, siye kama hawa;Maana ndiye aliyeviumba vitu vyote;Na Israeli ni kabila ya urithi wake;BWANA wa majeshi ndilo jina lake.
20. Wewe u rungu langu na silaha zangu za vita; kwa wewe nitawavunja-vunja mataifa; na kwa wewe nitaharibu falme;
21. na kwa wewe nitamvunja-vunja farasi, na yeye ampandaye; na kwa wewe nitalivunja-vunja gari la vita, na yeye achukuliwaye ndani yake;
22. na kwa wewe nitawavunja-vunja mwanamume na mwanamke; na kwa wewe nitawavunja-vunja mzee na mtoto; na kwa wewe nitawavunja-vunja kijana mwanamume na kijana mwanamke;
23. na kwa wewe nitamvunja-vunja mchungaji na kundi lake; na kwa wewe nitamvunja-vunja mkulima na jozi yake ya ng’ombe; na kwa wewe nitawavunja-vunja maliwali na maakida.
24. Nami nitamlipa Babeli, na wote wakaao ndani ya Ukaldayo, mabaya yao yote, waliyoyatenda katika Sayuni mbele ya macho yenu, asema BWANA.
25. Tazama, mimi ni juu yako, Ee mlima uharibuo, asema BWANA; wewe uiharibuye dunia nzima; nami nitaunyosha mkono wangu juu yako, na kukufingirisha chini toka majabalini; nami nitakufanya kuwa mlima ulioteketezwa.
26. Wala hawatatwaa kwako jiwe moja liwe la pembeni, wala jiwe moja liwe msingi; bali wewe utakuwa ukiwa daima, asema BWANA.
27. Itwekeni bendera katika nchi, pigeni tarumbeta kati ya mataifa, yawekeni mataifa tayari juu yake; ziiteni juu yake falme za Ararati, na Mini, na Ashkenazi; agizeni jemadari juu yake; wapandisheni farasi, kama tunutu.
28. Wekeni mataifa tayari juu yake, wafalme wa Wamedi, na maliwali wake, na maakida wake, na nchi yote ya mamlaka yake.
29. Nayo nchi yatetemeka, nayo ina utungu; maana makusudi ya BWANA juu ya Babeli yasimama, kuifanya nchi ya Babeli ukiwa, isikaliwe na mtu.
30. Mashujaa wa Babeli wameacha kupigana;Wanakaa katika ngome zao;Ushujaa wao umewapungukia;Wamekuwa kama wanawake;Makao yake yameteketea;Makomeo yake yamevunjika.