Yer. 50:20-40 Swahili Union Version (SUV)

20. Katika siku hizo na wakati huo, asema BWANA, uovu wa Israeli utatafutwa, wala uovu hapana; na dhambi za Yuda zitatafutwa, wala hazitaonekana; maana nitawasamehe wale niwaachao kuwa mabaki.

21. Panda juu ya nchi ya Merathaimu, naam, juu yake, na juu yao wakaao Pekodi; ua, ukaangamize nyuma yao, asema BWANA, ukatende kama nilivyokuagiza, yote pia.

22. Pana mshindo wa vita katika nchi,Mshindo wa uharibifu mkuu.

23. Imekuwaje nyundo ya dunia yoteKukatiliwa mbali na kuvunjwa?Imekuwaje Babeli kuwa ukiwaKatikati ya mataifa?

24. Nimekutegea mtego, Ee Babeli, nawe ukanaswa, nawe ulikuwa huna habari; umeonekana, ukakamatwa, kwa sababu ulishindana na BWANA.

25. BWANA amefungua akiba yake ya silaha, naye amezitoa silaha za ghadhabu yake; maana Bwana, BWANA wa majeshi, ana kazi atakayofanya katika nchi ya Wakaldayo.

26. Njoni juu yake toka mpaka ulio mbali;Zifungueni ghala zake;Mfanyeni kuwa magofu na kumharibu kabisa;Msimsazie kitu cho chote.

27. Wachinjeni mafahali wake wote;Na watelemkie machinjoni;Ole wao! Maana siku yao imewadia,Wakati wa kujiliwa kwao.

28. Sauti yao wakimbiao na kuokoka,Kutoka katika nchi ya Babeli,Ili kutangaza Sayuni kisasi cha BWANA, Mungu wetu,Kisasi cha hekalu lake.

29. Waiteni wapiga mishale juu ya Babeli,Naam, wote waupindao upinde;Pangeni hema kumzunguka pande zote;Ili asiokoke hata mtu mmoja wao;Mlipeni kwa kadiri ya kazi yake;Mtendeni sawasawa na yote aliyoyatenda;Kwa sababu amefanya kiburi juu ya BWANA,Juu yake aliye Mtakatifu wa Israeli.

30. Kwa sababu hiyo vijana wake wataanguka katika njia kuu zake, na watu wake wa vita, wote pia, watanyamazishwa katika siku hiyo, asema BWANA.

31. Tazama, mimi ni juu yako, Ewe mwenye kiburi, asema Bwana, BWANA wa majeshi; maana siku yako imewadia, wakati nitakapokujilia.

32. Na mwenye kiburi atajikwaa, na kuanguka, wala hapana atakayemwinua; nami nitawasha moto katika miji yake, nao utawala wote wamzungukao pande zote.

33. BWANA wa majeshi asema hivi, Wana wa Israeli, na wana wa Yuda, wameonewa pamoja; na wote waliowachukua mateka wanawashika sana; wanakataa kuwaacha.

34. Mkombozi wao ni hodari; BWANA wa majeshi ndilo jina lake; yeye atawatetea kwa bidii, apate kuistarehesha nchi, na kuwasumbua wakaao katika Babeli.

35. Upanga u juu ya Wakaldayo, asema BWANA, na juu yao wakaao Babeli, na juu ya wakuu wake, na juu ya watu wake wenye hekima.

36. Upanga u juu ya hao wajisifuo, nao watapumbazika; upanga u juu ya mashujaa wake, nao watafadhaika.

37. Upanga u juu ya farasi zao, na juu ya magari yao ya vita; na juu ya watu wote waliochanganyika ndani yake, nao watakuwa kama wanawake; upanga u juu ya hazina zake, nazo zitaibwa.

38. Ukosefu wa mvua u juu ya maji yake, nayo yatakaushwa; maana ni nchi ya sanamu za kuchongwa, nao wameingiwa na wazimu kwa ajili ya sanamu.

39. Basi, wanyama wakali wa jangwani, pamoja na mbwa-mwitu, watakaa huko, na mbuni watakaa ndani yake; wala haitakaliwa na watu milele; wala hapana mtu atakayekaa huko tangu kizazi hata kizazi.

40. Kama vile vilivyotokea Mungu alipoangusha Sodoma na Gomora, na miji iliyokuwa karibu nayo, asema BWANA; kadhalika hapana mtu atakayekaa huko, wala hapana mwanadamu atakayekaa huko kama wageni wakaavyo.

Yer. 50