15. Mpigieni kelele pande zote; amejitoa;Maboma yake yameanguka, kuta zake zimebomolewa;Kwa maana ni kisasi cha BWANA; mlipizeni kisasi;Kama yeye alivyotenda, mtendeni yeye.
16. Mpanzi mkatilie mbali na Babeli,Naye ashikaye mundu wakati wa mavuno;Kwa sababu ya kuuogopa upanga uoneao,Watageuka kila mtu kwa watu wake,Nao wataikimbilia kila mmoja nchi yake.
17. Israeli ni kondoo aliyetawanywa; simba wamemfukuzia mbali; kwanza mfalme wa Ashuru amemla, na mwisho Nebukadreza huyu, mfalme wa Babeli, amemvunja mifupa yake.
18. Basi, BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Tazama, mimi nitamwadhibu mfalme wa Babeli, na nchi yake, kama nilivyomwadhibu mfalme wa Ashuru.
19. Nami nitamleta Israeli tena malishoni kwake, naye atalisha juu ya Karmeli, na Bashani, na nafsi yake itashiba juu ya milima ya Efraimu, na katika Gileadi.
20. Katika siku hizo na wakati huo, asema BWANA, uovu wa Israeli utatafutwa, wala uovu hapana; na dhambi za Yuda zitatafutwa, wala hazitaonekana; maana nitawasamehe wale niwaachao kuwa mabaki.