Yer. 50:10-26 Swahili Union Version (SUV)

10. Nao Ukaldayo utakuwa mateka; wote wautekao watashiba, asema BWANA.

11. Kwa sababu mnafurahi, kwa sababu mnashangilia, enyi mnaouteka urithi wangu, kwa sababu mmewanda kama mtamba akanyagaye nafaka, nanyi mnalia kama farasi wenye nguvu;

12. mama yenu atatahayarika sana; yeye aliyewazaa atafadhaika; tazama, atakuwa taifa lililo nyuma katika mataifa yote, atakuwa jangwa, nchi ya ukame, na nyika.

13. Kwa sababu ya ghadhabu ya BWANA haitakaliwa na mtu, bali itakuwa ukiwa mtupu; kila mtu apitaye karibu na Babeli atashangaa, atazomea kwa sababu ya mapigo yake yote.

14. Jipangeni juu ya Babeli pande zote,Ninyi nyote mpindao upinde;Mpigeni, msiuzuie hata mshale mmoja;Kwa maana amemtenda BWANA dhambi.

15. Mpigieni kelele pande zote; amejitoa;Maboma yake yameanguka, kuta zake zimebomolewa;Kwa maana ni kisasi cha BWANA; mlipizeni kisasi;Kama yeye alivyotenda, mtendeni yeye.

16. Mpanzi mkatilie mbali na Babeli,Naye ashikaye mundu wakati wa mavuno;Kwa sababu ya kuuogopa upanga uoneao,Watageuka kila mtu kwa watu wake,Nao wataikimbilia kila mmoja nchi yake.

17. Israeli ni kondoo aliyetawanywa; simba wamemfukuzia mbali; kwanza mfalme wa Ashuru amemla, na mwisho Nebukadreza huyu, mfalme wa Babeli, amemvunja mifupa yake.

18. Basi, BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Tazama, mimi nitamwadhibu mfalme wa Babeli, na nchi yake, kama nilivyomwadhibu mfalme wa Ashuru.

19. Nami nitamleta Israeli tena malishoni kwake, naye atalisha juu ya Karmeli, na Bashani, na nafsi yake itashiba juu ya milima ya Efraimu, na katika Gileadi.

20. Katika siku hizo na wakati huo, asema BWANA, uovu wa Israeli utatafutwa, wala uovu hapana; na dhambi za Yuda zitatafutwa, wala hazitaonekana; maana nitawasamehe wale niwaachao kuwa mabaki.

21. Panda juu ya nchi ya Merathaimu, naam, juu yake, na juu yao wakaao Pekodi; ua, ukaangamize nyuma yao, asema BWANA, ukatende kama nilivyokuagiza, yote pia.

22. Pana mshindo wa vita katika nchi,Mshindo wa uharibifu mkuu.

23. Imekuwaje nyundo ya dunia yoteKukatiliwa mbali na kuvunjwa?Imekuwaje Babeli kuwa ukiwaKatikati ya mataifa?

24. Nimekutegea mtego, Ee Babeli, nawe ukanaswa, nawe ulikuwa huna habari; umeonekana, ukakamatwa, kwa sababu ulishindana na BWANA.

25. BWANA amefungua akiba yake ya silaha, naye amezitoa silaha za ghadhabu yake; maana Bwana, BWANA wa majeshi, ana kazi atakayofanya katika nchi ya Wakaldayo.

26. Njoni juu yake toka mpaka ulio mbali;Zifungueni ghala zake;Mfanyeni kuwa magofu na kumharibu kabisa;Msimsazie kitu cho chote.

Yer. 50