2. Basi, kwa sababu hiyo, tazama, siku zinakuja, asema BWANA, nitakaposikizisha mshindo wa vita juu ya Raba, mji wa Amoni, nao utakuwa magofu ya ukiwa, na binti zake watateketezwa kwa moto; ndipo Israeli watawamiliki wao waliokuwa wakimmiliki, asema BWANA.
3. Piga yowe, Ee Heshboni,Kwa maana Ai umeangamizwa;Lieni, enyi binti za Raba,Mjivike nguo za magunia;Ombolezeni, mkipiga mbioHuko na huko kati ya maboma;Maana Malkamu atakwenda kuhamishwa,Makuhani wake na wakuu wake pamoja.
4. Mbona unajisifu kwa sababu ya mabonde, bonde lako litiririkalo, Ee binti mwenye kuasi? Utumainiaye hazina zako, ukisema, Ni nani atakayenijilia?
5. Tazama, nitaleta hofu juu yako, asema Bwana, BWANA wa majeshi, itakayotoka kwa wote wakuzungukao; nanyi mtafukuzwa nje, kila mtu mbali kabisa, wala hapana mtu wa kuwakusanya wapoteao.
6. Lakini baada ya hayo nitawarudisha wana wa Amoni walio utumwani, asema BWANA.
7. Habari za Edomu. BWANA wa majeshi asema hivi, Je! Hapana tena hekima katika Temani? Mashauri yamewapotea wenye busara? Je! Imetoweka hekima yao?
8. Kimbieni, rudini nyuma, kaeni chini sana, enyi mnaokaa Dedani; maana nitaleta msiba wa Esau juu yake, wakati nitakapomwangalia.
9. Je! Kama wachuma zabibu wangekujia, wasingeacha zabibu ziokotwe? Kama wangekujia wevi usiku, wasingeharibu hata watakapopata vya kutosha?
10. Lakini nimemwacha Esau hana kitu, nimepafunua mahali pake pa siri, wala hataweza kujificha; kizazi chake kimeangamizwa, na ndugu zake, na jirani zake, naye mwenyewe hayuko.
11. Waache watoto wako wasio na baba, mimi nitawahifadhi hai, na wajane wako na wanitumaini mimi.
12. Maana BWANA asema hivi, Tazama, wale wasioandikiwa kunywea kikombe, watakinywea, ni hakika; na wewe je! U mtu ambaye hataadhibiwa kabisa? Hukosi utaadhibiwa, naam, kunywa utakunywa.
13. Kwa maana nimeapa kwa nafsi yangu, asema BWANA, kwamba Bozra utakuwa ajabu, na aibu, na ukiwa, na laana; na miji yake yote itakuwa ukiwa wa daima.
14. Nimepata habari kwa BWANA,Na mjumbe ametumwa kati ya mataifa,Akisema, Jikusanyeni, mkaujie,Mkainuke kwenda vitani.
15. Maana nimekufanya mdogo kati ya mataifa,Na kudharauliwa katika watu.
16. Katika habari za kuogofya kwako,Kiburi cha moyo wako kimekudanganya,Wewe ukaaye katika pango za majabali,Ushikaye kilele cha milima;Ujapofanya kioto chako juu sana kama tai,Nitakushusha kutoka huko; asema BWANA.
17. Na Edomu atakuwa ajabu; kila mtu apitaye atashangaa, na kuzomea, kwa sababu ya mapigo yake yote.
18. Kama vile vilivyotokea wakati wa kuangushwa Sodoma na Gomora, na miji iliyokuwa karibu nayo, asema BWANA; hapana mtu atakayekaa huko, wala hapana mwanadamu atakayekaa huko kama mgeni akaavyo.
19. Angalia, atapanda kama simba toka kiburi cha Yordani juu ya malisho yasiyonyauka; lakini nitamkimbiza ghafula ayaache; na yeye aliye mteule nitamweka juu yake; maana ni nani aliye kama mimi? Tena ni nani atakayeniandikia muda? Tena ni mchungaji yupi atakayesimama mbele zangu?