1. Habari za wana wa Amoni. BWANA asema hivi, Je, Israeli hana wana? Je! Hana mrithi? Basi, mbona Malkamu anamiliki Gadi, na watu wake wanakaa katika miji yake?
2. Basi, kwa sababu hiyo, tazama, siku zinakuja, asema BWANA, nitakaposikizisha mshindo wa vita juu ya Raba, mji wa Amoni, nao utakuwa magofu ya ukiwa, na binti zake watateketezwa kwa moto; ndipo Israeli watawamiliki wao waliokuwa wakimmiliki, asema BWANA.
3. Piga yowe, Ee Heshboni,Kwa maana Ai umeangamizwa;Lieni, enyi binti za Raba,Mjivike nguo za magunia;Ombolezeni, mkipiga mbioHuko na huko kati ya maboma;Maana Malkamu atakwenda kuhamishwa,Makuhani wake na wakuu wake pamoja.
4. Mbona unajisifu kwa sababu ya mabonde, bonde lako litiririkalo, Ee binti mwenye kuasi? Utumainiaye hazina zako, ukisema, Ni nani atakayenijilia?
5. Tazama, nitaleta hofu juu yako, asema Bwana, BWANA wa majeshi, itakayotoka kwa wote wakuzungukao; nanyi mtafukuzwa nje, kila mtu mbali kabisa, wala hapana mtu wa kuwakusanya wapoteao.
6. Lakini baada ya hayo nitawarudisha wana wa Amoni walio utumwani, asema BWANA.
7. Habari za Edomu. BWANA wa majeshi asema hivi, Je! Hapana tena hekima katika Temani? Mashauri yamewapotea wenye busara? Je! Imetoweka hekima yao?
8. Kimbieni, rudini nyuma, kaeni chini sana, enyi mnaokaa Dedani; maana nitaleta msiba wa Esau juu yake, wakati nitakapomwangalia.