5. Wakamwambia Yeremia, BWANA na awe shahidi wa kweli na uaminifu kati yetu; ikiwa hatufanyi sawasawa na neno lile, ambalo BWANA, Mungu wako, atakutuma utuletee.
6. Likiwa jema, au likiwa baya, sisi tutaitii sauti ya BWANA, Mungu wetu, ambaye tunakutuma kwake; ipate kuwa faida yetu, tunapoitii sauti ya BWANA, Mungu wetu.
7. Ikawa, baada ya siku kumi, neno la BWANA likamjia Yeremia.
8. Ndipo akamwita Yohana, mwana wa Karea, na maakida wote wa majeshi waliokuwa pamoja naye, na watu wote tangu wadogo hata wakubwa,
9. akawaambia, BWANA, Mungu wa Israeli, ambaye mlinituma kwake, ili niyaweke maombi yenu mbele yake, asema hivi;
10. Ikiwa mtakaa bado katika nchi hii, ndipo nitawajenga, wala sitawabomoa, nami nitawapanda, wala sitawang’oa; kwa maana nayajutia mabaya niliyowatenda.
11. Msimwogope mfalme wa Babeli, mnayemwogopa; msimwogope, asema BWANA; maana mimi ni pamoja nanyi, niwaokoe, na kuwaponya na mkono wake.
12. Nami nitawapa rehema, kwamba awarehemu ninyi, na kuwarudisha mkae katika nchi yenu wenyewe.
13. Lakini mkisema, Hatutaki kukaa katika nchi hii; msiitii sauti ya BWANA, Mungu wenu;